KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Wednesday, November 25, 2009
Mataifa makubwa duniani yamerasimu azimio litakalopigiwa kura na Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki baadae wiki hii ambalo linailani Ir
Mataifa makubwa duniani yamerasimu azimio litakalopigiwa kura na Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki baadae wiki hii ambalo linailani Iran kwa kuuficha mtambo wake wa pili wa kurutubisha uranium.
Mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Uingereza,China,Ufaransa,Urusi na Marekani pamoja na Ujerumani wameandaa rasimu ya azimio hilo ambalo litawasilishwa kwa bodi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA katika mkutano wao wa siku mbili unaoanza hapo kesho.
Lakini kwa mujibu wa wanadiplomasia bado hakuna uhakika iwapo rasimu hiyo itaweza kuungwa mkono na wajumbe wengi wa bodi hiyo katika mazungumzo kabla ya mkutano wao kwa hiyo mataifa hayo sita hatimae yumkini yakaamua kutoa azimio hilo kama taarifa tu badala ya kutaka lipigiwe kura.
Shirika la IAEA halikupitisha azimio juu ya Iran tokea mwezi wa Februari mwaka 2006.Lakini tangazo la kushtua la Iran hapo mwezi wa Septemba kwamba imekuwa ikijenga mtambo wa pili wa kurutubisha uranium kwa kukaidi vikwazo vya Umoja wa Mataifa kusitisha kabisa urutubishaji huo limeikasirisha hata Urusi na China ambazo huko nyuma zilikuwa zikisita sita kujiunga na wito wa mataifa ya magharibi kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi.
Mataifa hayo sita yalikutana mjini Brussels wiki iliopita ambapo walifikia makubaliano makubwa juu ya uzito wa tangazo hilo la karibuni la Iran.
Iran iliijulisha IAEA hapo mwezi wa Septemba kwamba imejenga mtambo wa pili wa kurutubisha madini ya uranium ndani ya mlima karibu na mji wa Qom na kuzusha shutuma mpya kutoka kwa mataifa ya magharibi juu ya mpango wake huo wa nuklea juu ya kwamba Iran inakanusha kwamba inajaribu kutengeneza bomu la nyuklia.
Iran imekuwa ikirutubisha uranium kwa miaka kadhaa kwenye mtambo katika mji wa kati wa Natanz kwa kukaidi vikwazo vilivyowekwa mara tatu na Umoja wa Mataifa dhidi yake.Madini ya uranium yanatumiwa kwa ajili ya nishati ya mitambo ya shughuli za kiraia lakini kwa uranium inayorutubishwa kwa hali ya juu inaweza kutumiwa kwa ajili ya kutengeneza mabomu ya atomiki.
Katika ziara yake ya Mashariki ya Kati waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ambaye nchi yake ni mojawapo ya nchi sita zinazoishinikiza Iran kusitisha mpango wake huo hapo jana akiwa nchini Israel amesema kwamba ni jambo lisilokubalika kwa Iran kumiliki silaha za nyuklia.
Katika repoti yake ya kwanza tokea wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA kukagua mtambo wa Qom mwezi uliopita shirika hilo limelalamika kwamba kuchelewa kwa Iran kutangaza kuwepo kwa mtambo huo hakusaidii kujenga imani.
Iran imesema mtambo huo ulikuwa umepangwa uwe mbadala iwapo mtambo wa Natanz utashambuliwa kwa mabomu.
Wakati haya yanajiri Rais Mahmoud Ahmeadinejad wa Iran amewasili Caracas Venezuela kwa mkutano na Rais Hugo Chavez masaa machache baada ya kiongozi huyo wa Iran kutua kwa muda mjini La Paz kwa mkutano na Rais wa Bolivia.
Ahmadinejad na Chavez viongozi wawili wanaopingana na Marekani ambao nchi zao ni wazalishaji wakubwa wa mafuta wanakutana leo hii kwa lengo la kuongeza ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Vyama vya upinzani na jumuiya Wayahudi wameishutumu ziara hiyo ya Ahmadinejad nchini Venezuela kutokana na kiongozi huyo kukanusha kutokea kwa maangamizi ya Wayahudi,ukiukaji wa haki za binadamu na mpango wake huo wa nyuklia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment