KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, June 3, 2009

Kashfa yayumbisha siasa za Uingereza




Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza anatazamiwa kujiuzulu huku kimbunga kikali cha kashfa ya marupurupu kikiendelea kuikumba serikali pamoja na bunge zima la Uingereza.

Kashfa kuhusu marupurupu wanayodai wabunge wa Uingereza imezusha zogo kubwa Uingereza huku majina ya viongozi mbalimbali yakimiliki vyombo vya habari.

Wabunge kadha wameamua kujiuzulu huku wengine wakiahidi kutotetea nyadhifa zao katika uchaguzi mkuu ujao.

Jacqui Smith alikuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani. Lakini duru zasema ingawa ameamua kuondoka kama waziri atasalia kuwa mbunge hadi uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya madai yaliyomtia matatani Bi Smith ni fidia kwa gharama ya mume wake kutizama filamu ya kimapenzi.

Waziri Mkuu Gordon Brown anatazamiwa kutangaza mabadiliko katika serikali yake baada ya uchaguzi wa bunge la Ulaya na serikali za mtaa ya Uingereza.

Wakati huo huo, chama tawala cha Labour kimewafungia mlango wabunge wake wanne kutowania tena viti vya ubunge katika uchaguzi ujao.

Inahofiwa kwamba viongozi zaidi serikalini, miongoni mwao Waziri wa Fedha Alistair Darling, wataondoka wakati wa mabadiliko hayo.

No comments:

Post a Comment