KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, January 29, 2011

Polisi watawanya wanafunzi Tanzania

Wanafunzi chuo kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania wamekabiliana na jeshi la Polisi baada ya kutaka kufanya maandamano ya kudai nyongeza ya posho wanayolipwa kwa siku kutoka shilingi elfu tano ifikie shilingi elfu kumi sawa na dola 8 kwa siku.

Ramani ya Tanzania


Maelfu ya wanafunzi walipanga kufanya maandamano hayo kwenda hadi Ikulu ili kupeleka malalamiko yao kwa Rais wa nchi hiyo Jakaya Kikwete.

Kuna taarifa ya wanafunzi wawili kujeruhiwa kutokana na tukio hilo kutoka Dar es Salaam mwandishi wetu John Solombi ametutumia taarifa ifatayo.

Wanafunzi hao wameunganisha madai yao ya nyongeza ya posho hiyo na suala la Serikali ya Tanzania kutaka kuilipa kampuni ya Dowans fidia iliyoshinda katika kesi ya kutakiwa kulipa dola za kimarekani milioni 64.

Wanafunzi hao walikuwa wamejiandaa na mabango.

Hata hivyo safari yao haikufika mbali kwani ghafla jeshi polisi lilifika na kuwasambaratisha kwa mabomu ya machozi pamoja na maji ya kuwasha.

Kamanda wa Polisi wa Kinondoni mjini Dar es Salaam Charles Kenyela amesema wametawanya maandamano hayo kwa kuwa wanafunzi hao hawakuwa na kibali cha kuandamana.

"Maandamano haya hayakuwa na baraka za chuo wala polisi". amesema kamanda Kenyela.

Kuna taarifa ya wanafunzi wawili kujeruhiwa kutokana na maandamano hayo kwa mujibu wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Yunus Mgaya.

Hadi jioni siku ya Ijumaa bado jeshi la Polisi lilikuwa likifanya doria ili kuwazuia wanafunzi hao kujikusanya tena na kufanya maandamano.

Kumekuwa na matukio ya mfulilizo wa migomo pamoja na maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania ambapo kuna taarifa za baadhi vyuo vingine vikuu vimekuwa na migomo ya kutoingia darasani kwa madai tofauti.

Suala la nyongeza ya posho wanayolipwa kwa siku, pamoja na kuchelewa kulipwa kwa wakati mikopo kutoka bodi ya mikopo ya Tanzania limekuwa likipigiwa kelele na wanafunzi wengi wa vyuo vikuu.

Tayari Serikali ya Tanzania kupitia waziri Mkuu Mizengo Pinda imekushaunda tume ili kuchunguza matatizo yanayowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania

No comments:

Post a Comment