KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, January 29, 2011

Bunge la Somalia lajiongezea muda zaidi

Wabunge wa Somalia wamepiga kura kuongeza muhula wao kwa miaka mitatu zaidi. Spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh Aden amesema hatua hii imefuatia pendekezo la shirika la IGAD kutaka serikali ya mpito kuongezewa muda.


Wajumbe wa serikali ya Somalia


Chini ya muafaka wa mwaka 2009, muda wa serikali ya mpito ya Somalia unamalizika Agosti mwaka huu.

Hii si mara ya kwanza kwa bunge la Somalia kujiongezea muda. Mwaka wa 2009 bunge hilo lilijiongezea miaka miwili ambayo inamalizika tarehe 20 mwezi wa Agosti 2011.

Lakini uamuzi wa sasa wa kujiongezea miaka mitatu zaidi, unatoa ujumbe kwamba Somalia itaendelea na mfumo wa mpito, badala ya mipango iliyojulikana awali ya kuanzisha serikali rasmi nchini humo.

Serikali iliyopo sasa ilitarajiwa kupitisha katiba mpya na kuandaa mfumo wa vyama vingi na uchaguzi, mambo ambayo hayaelekei kutendeka katika kipindi kifupi cha miezi saba ijayo.

Licha ya wabunge hao kujiongezea muda, hawakufafanua ni kwa nini walichukua uamuzi huo na malengo yao ya siku za baadaye, kwa vile hadi sasa hakuna jambo lolote muhimu walilofanya linaloweza kukumbukwa katika miaka sita iliyopita, tangu Bunge hilo lilipoanzishwa.

Mkuu wa kamati ya katiba katika Bunge Abdulkadir Shaykh Ismail, alisema uamuzi huo ulifikiwa kutokana na mapendekezo ya Jumuiya ya kikanda ya IGAD,l akini mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga mwezi uliopita aliambia BBC walikuwa katika harakati za kuandaa mazingira ya serikali ya sasa kukabidhi madaraka kwa utawala mpya.

Kufuatia uamuzi huo wa kujiongezea muda, kabla ya mwezi August, bunge litachagua spika mpya na Rais Sharif atapewa fursa ya kugombea tena.

Serikali ya mpito ya Somalia inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa makundi ya Kiislam kama vile Al-Shabab na hata usaidizi ambao serikali inapata kutoka kwa vikosi vya Muungano wa Afrika, haujazaa matunda ya kuwafurusha wanamgambo hao wanaodaiwa na uhusiano na kundi la Al Qaidah.

Balozi maalum wa Umoja wa Mataifa amekasirishwa na hatua ya kujiongezea muda iliyochukuliwa na bunge la Somalia.

Balozi Augustine Mahiga amesema kwa Wabunge kujiongezea muda wa miaka mitatu zaidi ni kuonyesha ubinafsi na hatari kwa mustakabali wa nchi.

No comments:

Post a Comment