KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, December 11, 2010

Zitto Kabwe Akaribishwa NCCR Mageuzi


CHAMA cha NCCR Mageuzi kimefungua milango kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zitto Kabwe.
Kauli hii imetolewa na chama NCCR Mageuzi katika kipindi hiki ambacho mustakabali wa mtendaji huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini umekuwa katika hali ya sitofahamu kufuatia chama Chadema kumpa barua ya kujieleza kutokana na kuwa katika orodha ya wabunge walioshindwa kujitokeza siku ya tukio la wabunge wa chama hicho kususia hutoba ya Rais Jakaya Kikwete.

Faustine Sungura ambaye ni Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi wa NCCR Mageuzi alisema, hatua ya kumkaribisha Zitto inatokana na ukweli kuwa ni mmoja wa wanasiasa nchini ambaye wana mchango mkubwa katika kambi ya upinzani.

Alisema kuwa, hatua hii ya kumfungulia milango Zitto haina maana kufurahia migogoro ndani ya chama chohote cha upinzani, bali wanachokiangalia ni aina ya wanasiasa na utendaji wao wa kazi hasa katika nia ya kuimarisha upinzani nchini.

Aliongeza kuwa, walifanya hivyo awali kwa kumkaribisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Leticia Musori kutokana na kuridhika na utendaji wake wa masuala ya kisiasa na watafanya hivyo iwapo Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini atafukuzwa ama kuonyesha nia ya kukihama chama chake.

Alibaisha Sungura kuwa, chama chake kipo katika kusimamia utendaji zaidi na kupatikana kwa wanasiasa wenye uwezo wa kujenga hoja na kuzitetea kama Zitto Kabwe kutaendeleza juhudi za NCCR Mageuzi za kukiimarisha chama kwa ajili chaguzi zijazo.

"Kwa kweli tumesikia misukosuko ambayo inampata Zitto kwa misimamo yake hivyo natumia fursa hii kumkaribisha NCCR ili aweze kutekeleza malengo yake ya kisiasa," alisema Sungura na kuongeza.

"Hatupo hapa kuona vyama vya upinzani vinakuwa na migogoro isiyokuwa na ulazima, tunapinga na kukemea mizozo inayoboa upinzani, ila tupo tayari kufanya kazi na mwanasiasa yeyote mwenye kutetea maslahi ya nchi kupitia kambi ya upinzani".

Aliongeza kuwa, wameridhika na utendaji kazi wa wanasiasa waliojiunga na chama chao hivi karibuni na kazi iliyo mbele yao ni kuona chama kinaimarika zaidi nchini na matarajio ya baadae ni kuendelea kupata viti vingi vya ubunge na udiwani.

Katika hatua nyingine Sungura alisema Halmashauri Kuu ya chama hicho inatarajia kukutana Desemba 11 mwaka huu kwa madhumuni ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini ya hali ya kisiasa mara baada ya kuamlizika kwa Uchaguzi Mkuu uliopita

No comments:

Post a Comment