KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Tuesday, December 14, 2010

Waumini RC Rukwa 'wakiri' kukashifu


Geofrey Nyang'oro, Sumbawanga
KUTENGWA kwa waumini wa Kanisa Katoliki wilayani Sumbawanga ambao walitengwa mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kunaweza kuhusishwa na masuala ya kisiasa, lakini imebainika kuwa walinajisi kanisa katika kusherehekea ushindi wa kisiasa, Mwananchi inakuthibitishia.Habari za kutengwa kwa waumini hao zilihusishwa sana na purukushani za uchaguzi mkuu na ilidaiwa kuwa walitengwa na kanisa kutokana na kujihusisha na chama tawala cha CCM, lakini Mwananchi ilifanya utafiti na kubaini kuwa waliofungiwa wengi wamegundua kosa lao na sasa wanalijutia

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Sumbawanga mkoani Rukwa umebaini kuwepo kwa vitendo vya kukashifu imani ya Kikristo vilivyofanywa na baadhi ya waumini hao wakati wa kampeni na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31.

Mwananchi imebaini kuwa waumini hao walitengeneza jeneza na ndani yake wakaweka mgomba na sanamu ya kanisa na msalaba wake na baadaye kulizika jeneza hilo.
Tukio hilo lilifanyika katika kijiji cha Chelenganya kilicho umbali unaokadiriwa kuwa ni zaidi ya kilometa 20 kutoka yalipo makao makuu ya Manispaa ya Sumbawanga.

Muumini mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alilimbia gazeti hili kijijini hapo kuwa siku ya tukio baadhi ya waumini walitengeneza jeneza na kuweka mgomba ndani yake pamoja na sanamu ya kanisa na msalaba baadaye kufanya ibada ya mazishi, kitu ambacho kinaonekana kuwa ni kuikashifu imani ya Kikristo.
Alisema kibaya zaidi ni kitendo cha waumini hao kuingia kanisani wakiwa na jeneza hilo na kuendesha ibada ya mazishi kabla ya kwenda kulizika jeneza hilo.

Alisema mgomba ulitumika kama ishara ya kumzika mgombea wa Chadema, Norbet Yasebo wakati waliweka msalaba na kanisa kama ishara ya vilitabiriwa kama mazishi ya kanisa hilo ambalo inadaiwa kuwa lilikuwa likimuungano mgombea huyo wa chama cha upinzani.
Lakini waumini hao sasa wanajutia kitendo chao.

Wanajitetea kuwa walifanya hivyo bila kujua kuwa walikuwa wakifanya kosa kubwa kwa kanisa lao; walifikiri wapo kwenye shamra shamra za kusherehekea ushindi wa mgombea wao.
"Hatukujua kama hili tulilokuwa tukilifanya ni kosa, bali tulikuwa tukisherehekea ushindi wa mgombea wetu ambaye alishinda katika uchaguzi huu," alisema mmoja wa waumini hao waliotengwa kijijini hapo huku akitaka jina lake lisiandikwe gazetini.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Sumbawanga, Charles Kabanga alithibitisha kuwepo kwa waumini wa kanisa hilo waliotoa kashfa kwa kanisa na mapadri wao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita Oktoba 31.
Kabanga, ambaye naye ni miongoni mwa waumini wa kanisa hilo waliotengwa kutokana na madai ya kuhusika katika vitendo hivyo, alisema wakati wa kampeni aliwashuhudia baadhi ya Wakristu wakitoa kashfa kwa mapadiri hao kwa madai kuwa wanamkashifu mgombea wao wakati wao pia wana mapungufu yao.

Alisema waumini hao, ambao wengi ni wajumbe wa CCM, waliwataka mapadri kuwaachia suala la kisiasa na kwamba wandelea na kazi yao ya kuhubiri neno la Mungu.
"Wanaosema mimi nilihusika na kitendo cha kuwakashifu na kuwatukana mapadri wangu wananionea," alisema Kabanga.
"Kilichotokea ni kwamba nilikuta baadhi ya wajumbe CCM ambao pia ni waumini wa kanisa hilo wakisema mapadri wanamkashifu mgombea wetu kuwa ana tabia mbaya wakati wao wana mapungufu mengi," alisema Kabanga akiwanukuu waumini wenzake.

"Ndipo nilipoanza kuwatetea mapadiri wangu na kuwaambia watu hao waache kuzungumza hayo kwa kuwa sote ni wakirstu swa Kanisa Katoliki na hao ni mapadiri wetu ambao hutupatia huduma za kiroho. Niliwaambia kuwa hata wakisema hivyo leo, padri ni padri na ataendelea kuwahudumia," alisema Kabanga.
Alisema katika mkutano huo aliwaomba waumini wenzake kuacha kuwakashifu mapadiri, badala yake kuendelea kufuata misingi ya imani ya kanisa hilo huku wakisikiliza mafundisho yao na kuacha kufauata matendo wanaoyofikiri yapo kinyume na mwenendo na maadili ya mapadri hao.

Kuhusu suala la mgombea wa CCM kukufuru utatu mtakatifu, yaani Mungu, mwana na roho, Kabanga alikanusha kuwepo na kitendo hicho na kueleza kuwa kauli zake zilitafsiriwa vibaya.
"Alichosema mgombea wetu ni kuhamasisha wanachama na wapenzi wake kuchugua mafiga matatu, mafiga matatu ambayo ni rais, mbunge na diwani na si vinginevyo," alisema Kabanga.
"Hata hivyo sisi kama chama tulimwita mgombea wetu na kumsihi kuacha kutumia maneno ambayo yanagusa imani kwenye kampeni zake," alisema Kabanga.

Kuhusu kutengwa kwake, Kabanga alisema uamuzi huo unamuuma na kumkosesha amani katika maisha yake ya sasa.
"Hata ninapokuwa njiani nikitembea, najisikia vibaya kwa jinsi waumini wenzangu wanavyoniangalia na jinsi wanavyozungumzia kuwa nimetengwa na kanisa," alisema.
Naye Chiritina Ninde, ambaye pia ametengwa na kanisa hilo, aliimbia Mwananchi kuwa mgombea wa chama hicho katika kampeni zake aliwataka wapiga kura kuchagua mafiga matatu ambayo ni rais, mbunge na diwani akirejea maandiko ya kwenye kitabu kitakatifu cha Biblia kuwa kuna nafsi tatu ambazo ni Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu ambazo Kikristo hutafsiriwa kuwa ni kitu kimoja.

Ninde, ambaye haruhusiwi kushiriki ibada, kupokea sakaramenti na huduma nyingine za kiroho zinazotolewa na kanisa hilo kutokana na kutengwa, anasema adhabu hiyo inamuumiza sana.
"Inauma sana mtu kutengwa na jumuiya uliyokuwa ukishiriki nayo katika kila kitu leo siruhusiwa kushiriki ibada wala kuhudhuria mazishi ya ndugu wala jamaa yangu ambaye kanisa litahusika... kwakweli hadi sasa sielewi cha kufanya," alisema huku akionyesha barua aliyokabidhiwa na kanisa la hilo Parokia ya Kirstu Mfalme Desemba 17.
"Mimi nimezaliwa na kudumu katika imani ya kanisa katoliki hadi sasa. Sijawahi kusikia tukio kama hilo tangu kuzaliwa kwangu na wala sikutegemea kama ingefikia siku nikatengwa na kanisa."

Baadhi ya waumini walilimbia gazeti hili kuwa chanzo cha mgogoro huo ni kitendo cha kanisa hilo kutoa elimu ya uraia wakati wa kampeni, likihamasisha waumini wake kuchagua viongozi bora.

Lakini elimu hiyo ilichukuliwa na wanachama wa CCM kuwa ililenga kumsaidia mgombea wa Chadema ambaye ni Mkristo.
"Kila mara mapadri walitumia muda mwingi kuhamasisha waumini kuchagua viongozi bora huku wakitoa sifa za mtu anayefaa kuwa kiongozi. Lakini sifa hizo zilionekana kumhusu mgombea wa Chadema jambo lililowafanya waumini hao kutafisiri kuwa mapadiri wanaipendelea Chadema," alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.
Akizungumzia hilo, Wakili wa kiaskofu wa kanisa hilo mjini Sumbawanga, Padri Modest Katonto alisema kanisa lilikuwa likitimiza wajibu wake wa kutoa elimu ya uraia kwa waumini wake kuhusu uchaguzi na wala halikupendelea chama chochote.
"Katika kipindi hicho kanisa lilitoa elimu ya uraia kwa waumini wake sambamba na kukemea vitendo na mwenendo mbovu, na wala halikupendelea chama chochote cha siasa. Madai ya baadhi yao kuwa tulipendelea chama ni uzushi na uongo," alisema Katonto.

Alisisitiza kuwa kanisa litaendela kufundisha waumini wake juu ya kuwajibika katika kutenda mema.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Aeshy Hilaly aliibuka mshindi dhidi ya Yamsebo wa Chadema ambaye pia walikumbana kwenye kura za maoni ndani ya CCM kabla ya kuhamia upinzani.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Kanisa Katoliki Sumbawanga lilitangaza kuwatenga waumini wake wapatao 27 na kuwasimamisha waumini wengine zaidi ya 400 kwa madai ya kulikashifu kanisa na kukufuru.

Padri Katonto alitaja makosa yaliyolilazimu kanisa kufikia hatua hiyo kuwa ni pamoja na baadhi ya waumini kukufuru matumizi ya msalaba na kanisa kwa kutengeneza sanamu ya vitu hivyo na kuvizika.
Alitaja makosa mengine kuwa ni kitendo cha baadhi ya waumini kujihusisha na matusi, kejeli na maneno ya uchonganishi kwa viongozi wa kanisa na waumini wenzao.

Pia baadhi ya wagombea walidaiwa kujifafanisha na Mungu mwenye nafsi tatu, kitendo kinachoonekana kuwa ni kufuru kwa kanisa hilo linaloamini katika utatu mtakatifu.
Akifafanua kuhusu adhabu hizo, Padri Katonto alithibitisha uamuzi wa kanisa hilo kuwatenga waumini 27.
Padri Katonto alisema kwa mujibu wa sheria namba 1364 ya Kanisa Katoliki, kosa la waumini hao linawatenga na umoja wa kanisa bila ya kutangaziwa na uongozi wa kanisa.

Katonto alisema iwapo waumini hao watakwenda kwenye nyumba za ibada, watatakiwa kuondoka na kwamba ibada itasitishwa hadi hapo watakapoondoka na zaidi ikiwa watakufa bila kutubu hawatapata maziko na kanisa.

Alibainisha kuwa kundi la pili ni waumini waliowekewa pingamizi na kufafanua kuwa kundi hilo linanyimwa huduma za kanisa wakati makosa yake yakiendelea kuchunguzwa hadi hapo itakapobainika kuhusiaka au la.
Alisema baada ya uchunguzi kukamilika na kubaini watuhumiwa hawakuhusika basi muumini husika anarejeshewa huduma zote za kiroho.
Hata hivyo alisema waumini waliowekewa pingamizi ambao ni zaidi ya 400 wanaruhusiwa kuendelea kushiriki katika umoja na kanisa na si kama ilivyo kwa waliotengwa

No comments:

Post a Comment