KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Liyumba ashindwa kupangua hukumuHARAKATI za kigogo wa Zamani wa Benki Kuu (BoT), Amartus Liyumba kupangua hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela, jana iligonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kuamua aendelee kutumikia adhabu hiyo. Barua alizoziandika mkurugenzi huyo wa zamani wa utawala na fedha wa BOT kwenda kwa mshauri wa mradi wa ujenzi wa majengo ya ghorofa pacha kuhusu mabadiliko ya mradi huo, ndizo zilizomuweka matatani Liyumba katika rufaa yake.

Liyumba alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 24 mwaka 2010 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi. Hata hivyo, Mei 28 mwaka huo huo, kwa kutumia jopo la mawakili walioongozwa na Majura Magafu, Liyumba alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda akitoa sababu 12 za kupinga hukumu hiyo pamoja na adhabu.

Katika sababu zake za kupinga hukumu hiyo jopo la mawakili wa Liyumba, pamoja na mambo mengine lilisema kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria na kiukweli katika kutathmini ushahidi na utetezi na kwamba ilkiuka kanuni zilizowekwa na mahakama za juu katika kutoa adhabu.

Lakini katika hukumu yake ya jana, Jaji Emilian Mushi alitupilia mbali utetezi wa Liyumba na mawakili wake na akungana na hoja za upande wa mashtaka pamoja na hukumu ya Mahakama ya Kisutu. Katika hukumu hiyo yenye kurasa 60 aliyoisoma kwa muda wa saa 2:04, Jaji Mushi alisema:"Hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi." Jaji Mushi licha ya kukiri kuwa bodi ya wakurugenzi wa BoT iIipoteza nguvu katika za udhibiti wa maamuzi yanayohusu mradi wa ujenzi wa majengo hayo na kuburuzwa na menejimenti ya benki hiyo, alikubaliana na hoja za mawakili wa Liyumba kuwa bodi hiyo ilikuwa dhaifu.

Alisema licha ya bodi hiyo kujumuisha wanataaluma maarufu na wenye uzoefu, walionekana kutokuwa na msaada wowote mbele ya menejimenti hiyo. Hata hivyo, alipingana na hoja za mawakili hao kuwa mabadiliko ya mradi huo yalioongeza pia gharama za mradi, hayakuwa na athari kwa bodi hiyo na kwamba kama zingekuwepo athari hizo basi bodi hiyo ndio ingelaumiwa na siyo mrufani huyo.

Jaji Mushi alisema kuwa kosa lililomtia hatiani Liyumba si tu kwamba lilisababisha athari kwa BoT, bali pia kwa uchumi wa taifa kwa jumla.

Kabla ya kufikia hitimisho la hukumu yake hiyo, Jaji Mushi ilipigilia msumari wa mrufani huyo kuendelea kusota rumande. Jaji Mushi alianza kwa kufanya marejeo ya mwenendo mzima wa kesi ya msingi dhidi ya Liyumba. Alichambua ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi wa mshtakiwa pamoja na hukumu na adhabu iliyotelewa na Mahakama ya Kisutu na sababu zake, kisha akapitia sababu na hoja za rufaa na majibu ya hoja za mjibu rufaa (serikali).

Jaji Mushi, ambaye anaelezewa na baadhi ya mawakili kuwa ni mtaalamu wa kesi za makosa ya rushwa, uhujumu uchumi na ubadhirifu, alichambua hoja za pande zote, moja baada ya nyingine, kisha kuanza kuzitolea maamuzi. Jaji Mushi alizikataa hoja zote kwamba Mahakama ya Kisutu ilikosea katika kutathmini ushahidi na kufikia hukumu iliyomtia hatiani Liyumba, akisisitiza kuwa hukumu ilikuwa sahihi.

Pamoja na mambo mengine mawakili hao wa Liyumba walidai kuwa katika mradi huo, Liyumba alikuwa ni mratibu tu na kiungo kati ya menejimenti na mshauri wa mradi. Walidai kuwa mabadiliko ya mradi yalikuwa yakifanywa na menejimenti kwa maana ya gavana, na kwamba haikuwa rahisi kwa mrufani huyo kuweza kufanya maamuzi bila ridhaa ya gavana na bodi.

Liyumba alidai wakati akitoa ushahidi awali kuwa barua alizokuwa akiziandika kuhusu mabadiliko ya mradi, alikuwa akifanya hivyo kwa maelekezo ya mdomo kutoka kwa gavana wa wakati huo (marehemu Daudi Balali), maelezo ambayo yalipingwa na Mahakama ya Kisutu. Hata hivyo, Jaji Mushi alisisitiza kuwa hukumu ya kesi ya msingi ilikuwa sahihi kwa sababu mrufani huyo alikidhi viashiria ya kutenda kosa alilotiwa hatiani chini ya kifungu cha 96(1) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 na marekebnisho ya mwaka 2002.

Alivitaja vigezo hivyo ambavyo alisema havikubishaniwa na pande zote kuwa ni pamoja na mrufani kuwa mwajiriwa wa BoT, kwamba mradi ulikuwa chini ya usimamizi na uratibu wake. Alisema pia gharama za mradi zilitokana na bajeti ya benki hiyo ambayo bodi ya wakurugenzi ndio yenye mamlaka ya kuidhinisha na kwamba kulikuwa na mabadiliko ya mradi yaliyosababisha ongezeko la gharama.

Jaji Mushi alisema ingawa gavana ni sehemu ya menejimenti, si sahihi kusema kuwa yeye pekee ndiye menejimenti kama Liyumba na mawakili wake walivyodai na kwamba madaraka yake yana mpaka.

Akizungumzia barua alizoziandika Liyumba, Jaji Mushi alisema ingekuwa ni barua moja au mbili, ingeweza kuwa na mantiki kuwa alielekezwa na gavana kwa mdomo, lakini akasema si kwa barua zote nane. Alisema hata kama kungekuwa na ushahidi, gavana hana mamlaka hayo na hivyo asingekuwa na kinga kisheria.

Jaji Mushi alisisitiza kuwa Liyumba na Balali walikuwa wakijua sera, kanuni na taratibu za fedha za BoT, kwamba walipaswa kupata ridhaa ya bodi kabla ya kufanya mabadiliko, lakini walizipuuza pamoja na jukumu la Bodi.

Alisema Liyumba kama mtaalamu na mtawala miongoni mwa wajibu wake ulikuwa ni kumshauri gavana kusimama katika sera, kanuni, na taratibu za kifedha, lakini alimshawishi kuzipuuza.

Kuhusu hoja ya adhabu ya kifungo kama ilivyodaiwa na mawakili wa Liyumba kuwa Mahakama ya Kisutu ilivunja kanuni za kutoa adhabu kwa kuwa ilipaswa kutoa adhabu ya faini, Jaji Mushi alisema si kila kifungu kinachotoa adhabu zaidi ya moja ni lazima itolewe faini kwanza. Magafu akisaidiana na mawakili wengine, Jaji Hilary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo walidai kuwa mahakama hiyo ilimtia hatiani kimakosa.

Hata hivyo, Jaji Mushi alisema ingawa kanuni zinaelekeza hivyo, mahakama zinapewa uhuru wa kuchagua aina ya adhabu kutegemeana na maizingira ya kesi na kwamba kwa mazingira ya kesi hiyo adhabu hiyo ilikuwa ni sahihi.

“Katika mazingira ya kesi hii, naridhika kuwa Mahakama iliyosikiliza kesi hii ilikuwa sahihi kufikia hitimisho kuwa maslahi ya jamii hayatafikiwa kwa kutoa adhabu ya faini isipokuwa kifungo,” alisema Jaji Mushi. "Nimeridhika kuwa adhabu iliyotolewa kwa mrufani ilikuwa ni ya kisheria na haikuwa imezidi. Kwa kusema haya naridhika kwamba rufaa hii haina nguvu, na ninaitupilia mbali kabisa. Haki ya rufaa inatolewa,” alihitimisha Jaji Mushi

No comments:

Post a Comment