KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Kiingereza, kiswahili kinatesa watoto- Utafiti


Hussein Kauli
UTAFITI wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uwezo, umebaini kuwa idadi kubwa ya watoto nchini hawawezi kufaulu majaribio katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hesabu kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na kukosa ujuzi wa kufanya majaribio ya masomo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Grace Soko alisema kwa mujibu wa utafiti huo, watoto wengi nchini licha ya kwenda shule hawana stadi za msingi za kusoma kuandika na kuhesabu wanazotakiwa kuzipata.

Alisema utafiti huo uliofanywa katika wilaya 38 nchini kwa lengo la kujua uwezo wa wanafunzi katika shule za msingi, ulibaini kuwa wilaya ya Muleba inaongoza kwa kuwa na wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kujifunza.

Wilaya hiyo ya Muleba ilipata asilimia 22, 5, na 26 katika kujifunza Kiswahili, Kiingereza na Hesabu, ikifuatiwa na wilaya ya Kasulu iliyopata asilimia 25, 10, 18, katika masomo hayo.

Soko alitaja wilaya nyingine zilipata asilimia ndogo kuwa ni Mwanga, Shinyanga Mjini huku wilaya za Rombo, Ilemela, Mbulu, Moshi Mjini na Moshi Vijijini zikifanya vizuri katika kujifunza.

Alitoa mfano kwa kwa wanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya Muleba ambapo asilimia kumi tu wa darasa hilo ndio walioweza kusoma Kiswahili, asilimia 17 wanaweza kufanya hesabu za kuzidisha na asilimia mbili tu wanaweza kusoma Kiingereza.

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye wilaya ya Muleba, Rombo asilimia 63 ya wanafunzi wa darasa la tatu wanaweza kusoma Kiswahili,asilimia 24 wanaweza kusoma Kiingereza na na asilimia 39 wanaweza kufanya hesabu.

Alisema katika utafiti huo uliofanywa kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 5 hadi 16, mwanafunzi wa Rombo anaweza kufanya vizuri mara tatu ya mwanafunzi wa Muleba katika kusoma hadithi ya Kiswahili.

Aliongeza kuwa mwanafunzi wa Rombo anaweza kufanya vizuri zaidi hesabu za kuzindisha na anaweza kusoma hadithi ya Kiingereza vizuri zaidi ya mara nane ya usomaji wa mwanafunzi wa Muleba.

Hata hivyo, anasema wakati Rombo ikionekana kufanya vizuri kuliko wilaya zilizofanyiwa utafiti huo, karibu nusu ya watoto wote hawawezi kusoma Kiingereza.

Alisema pia nusu ya watoto katika wilaya hiyo hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha na karibu mtoto mmoja kati ya watoto watatu hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili.

Aliongeza kuwa kuna wilaya moja tu ya Rombo nchini kati ya wilaya zilizofanyiwa utafiti, ndiyo yenye angalau nusu ya watoto wa wanaoweza kufanya hesabu za kuzidisha.

“Hakuna wilaya hata moja iliyoonekana angalau kuwa na watoto wanaoweza kusoma hadithi ya Kiingereza kwani zilizoko zinaaznia asilimia 45 (Rombo) hadi ya chini asilimia 5(Muleba)” alisema Soko.

Alisema pamoja na hali hiyo,watoto wa wa darasa la tatu wenye umr wa miaka tisa hadi 16 au zaidi wanapaswa kuwa an uwezo wa kufanya majaribio ya darasa la pili, hali ambayo ni kinyume na matokeo ya utafiti huo.

Alisema katika wilaya hizo 38 wilaya za mijini kwa ujumla zilionekana kufanya vizuri ikilinganiswha na za vijijini ambapo wilaya za mijini zilikuwa juu ya nusu ya walaya zote isipokuwa wilaya za Morogoro na Tanga.

Hata hivyo, pamoja na wilaya za vijijini kuwa na ufaulu wa chini kulinganisha na za mijini, wilaya mbili bora za utafitu huo ni za vijijini ambazo ni Rombo na Mbulu

No comments:

Post a Comment