KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, December 14, 2010

Juhudi za kusaka amani Mashariki ya Kati



Großansicht des Bildes mit der Bildunterschrift: George Mitchell, na rais Mahmoud Abbas, wakati wa kikao chao Ukingo wa MagharibiWapalestina wasema hawawezi kuingia katika meza ya mazungumzo na Israel mpaka waache kujenga Ukingo wa Magharibi

Maafisa wa mamlaka ya wapalestina wamesema hapawezi kuweko mazungumzo na Israeli hadi nchi hiyo itakapoafiki agizo la kuitaka isimamishe ujenzi wa makaazi ya walowezi.Mpatanishi mkuu wa Palestina Saeb Erakat pia ametoa tamko kama hilo baada ya kufanyika mkutano kati ya mjumbe wa Marekani katika eneo hilo George Mitchell na rais Mahmoud Abbas.Ama kwa upande mwingine Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniya amesema kundi hilo haliwezi hata siku moja kuitambua Israel.

Mpatanishi mkuu wa Palasetina Saeb Erakat amewaambia waandishi wa habari kwamba Wapalestina hawawezi kukaa katika meza ya mazungumzo na Waisreli ikiwa nchi hiyo haitokubali kuzingatia sharti la kuitaka isimamishe ujenzi wake wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi.

Tamko hilo limetolewa kufuatia mkutano baina ya mjumbe wa Marekani na rais Mahmoud Abbas uliofanyika hii leo mjini Ramallah baada ya hapo jana pia kufanyika mazungumzo kama hayo huko Jerusalem kati ya Mitchell na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Washington,wizara ya mambo ya nje imeeleza kwamba Mitchell na waziri mkuu Netanyahu wamejadiliana kwa kina na kupata mwanga zaidi katika kupata njia bora ya kushughulikia masuala nyeti yatakayofikia lengo la kupatikana amani.

Mjumbe huyo wa Marekani amesema pamoja na kwamba Marekani imeshindwa kuizuia Israel isiendelee na mpango wake wa kujenga makaazi mapya katika ardhi ya Wapalestina lakini bado iko tayari kuongeza juhudi kuona kwamba kunapatikana dola la Wapalestina litakaloishi bega kwa bega na Israel kwa amani.

Kushindwa huko kwa Marekani kuizuia Israel isijenge katika ardhi ya Wapalestina inayoikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi ndiko kulikosababisha kuvunjika kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya kusaka amani wiki tatu baada ya kuanzishwa. Aidha Uongozi wa Palestina umetaka pia paitishwe mkutano wa dharura wa pande nne kuhusu mgogoro wake na Israel,mkutano utakaowashirikisha wajumbe wa Marekani Umoja wa Ulaya Urusi na Umoja wa Mataifa.

Katika jitihada nyingine za kutafuta njia nyingine ya kuyarudisha mazungumzo hayo hapo jana pia waziri wa Ulinzi wa Israeli Ehud Barak alikuwa na mkutano na mwenzake wa Marekani zaidi walijadiliana juu ya kitisho kinachosababishwa na Iran kutokana na mpango wake wa Kinuklia pamoja na hali ya sasa ya juhudi za amani katika eneo hilo la Mashariki ya kati.

Katika eneo la Gaza leo kundi la Hamas likiadhimisha miaka 23 ya kuasisiwa kundi hilo kiongozi wake Ismail Haniya amerudia tena kuusisitiza msimamo wake kwamba hawawezi kamwe kuitambua Israel.Kundi la Hamas liliundwa na Sheikh Ahmed Yassin Desemba 14 mwaka 1987 siku kadhaa baada ya kutokea vuguvugu la kwanza la Intifada dhidi ya Israel.

Mwandishi Saumu Mwasimba/DPE

Mhariri AbdulRahman

No comments:

Post a Comment