KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Jaji Mkuu agoma kujitoa kesi ya samaki 'wa Magufuli'


James Magai
JAJI Mkuu wa Tanzaia, Agustino Ramadhan, amepuuza maombi ya Serikali ya kumtaka ajiondoe katika jopo la majaji wanaosikiliza maombi ya dhamana ya washtakiwa katika kesi ya uvuvi haramu, katika Ukanda wa Bahari Kuu wa Tanzania.

Jaji Ramadhan, alitoa msimamo huo jana wakati kesi hiyo inayowakabili raia wa mataifa matano ya nje, ilipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa rufaa ya kupinga masharti ya dhamana ya washtakiwa hao.
Rufaa hiyo ya kupinga masharti ya dhamana kwa washtakiwa,ilifunguliwa Desemba 8 mwaka huu na jopo la mawakili wa washtakiwa hao, linaloongozwa na wakili Kapteni Ibrahimu Bendera, akisaidiwa na John Mapinduzi.

Katika maombi yao, mawakili hao wanaiomba mahakama hiyo, itangue uamuzi uliotolewa na Jaji Njengafibili Mwaikugile, kuhusu masharti ya dhamana.
Masharti hayo ni pamoja na kuwataka washtakiwa watoe mahakamani kiasi cha Sh1.37bilioni kila mmoja na kuwa na wadhamini wawili.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo iliyofikishwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoongozwa na Jaji Mkuu akisaidiwa na majaji Mbarouk Mbarouk na Othman Chande, upande wa serikali ulitoa hoja ya awali ya kumtaka Jaji Agustino ajiondoe katika kesi hiyo.

Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus, alisema hawana imani na Jaji Mkuu kwa kuwa aliwahi kutoa kauli iliyoonyesha kuwa ana maslahi katika kesi hiyo na kwamba kwa msingi huo, hatatenda haki.
Stanslaus alikuwa akirejea hotuba ya Jaji Mkuu ya Mei 25 mwaka huu kwa Waziri wa Katika na Katiba, Mathias Chikawe, wakati wa ufunguzi wa semina ya majaji mjini Arusha.

Katika hotuba hiyo, Jaji Mkuu aliwatetea washtakiwa hao kuwa kisheria hawakupaswa kushtakiwa wote bali nahodha wa meli yao waliyokuwa wakifanyia shughuli za uvuvi na kwamba wameshtakiwa kimakosa.
Pia Jaji Mkuu alizungumzia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kuhusu masharti ya dhamana kuwa haikuwa haki.
Hata hivyo Jaji Mkuu alipuuza hoja hizo za serikali za kumtaka ajitoe katika kesi hiyo na kwamba hawezi kujiondoa kwa kuwa hoja za serikali hazina msingi.

Kabla ya kutoa msimamo wake huo, Jaji Ramadhan alimtaka Wakili Stanslaus asome mwongozo wa uendeshaji wa shughuli za mahakama.
Mwongozo huo unabainisha kuwa Jaji Mkuu anaruhusiwa kutoa mwongozo au maelekezo kwa maofisa wake katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa mantiki ya mwongozo huo Jaji Mkuu alisema kuwa alichokifanya alikuwa akikifanya kama jaji mkuu ambaye ni kiongozi wa mhimili huo wa kusimimia utoaji wa haki.
Alimuliza wakili Boniface iwapo tangu atoe hotuba hiyo miezi saba iliyopita kuna athari zozote katika mwenendo wa kesi hiyo naye akajibu kuwa hakuna.

Akitoa uamuzi wake baada ya mjadala huo baina yake na mawakili hao wa serikali, Jaji Mkuu alisema kwa hoja hizo tu, hawezi kujitoa na kwamba sababu zaidi za kutokujitoa katika kesi hiyo atazitoa mwisho wa usikilizwaji wa rufaa hiyo kwenye hukumu yake.

Katika hatua nyingine upande wa serikali ulikiri kuwa Mahakama Kuu ilikosea katika hukumu yake kwa kuwaamuru washtakiwa hao kila mmoja atoe pesa taslimu Sh1.37 kwa ajili ya dhamana.
Baada ya kuigomea serikali kujiondoa katika kesi hiyo Jaji Ramadhan aliendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo hadi mwisho.

Katika hoja zao, mawakili wa upande wa utetezi walipinga masharti hayo na kuitaka mahakama
kutengua uamuzi wa masharti uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mawakili hao Kapteni Bendera na Mapinduzi walitoa maombi hayo mbele ya mahakama hiyo kwa madai kuwa kwa sasa meli iliyokamatwa ikidaiwa kutumiwa na watuhumiwa hao tayari iko mikononi mwa serikali na kwamba tayari samaki waliokamatwa katika meli hiyo walishagawiwa kwa wananchi.

Pia walisema kuwa hati ya mashtaka ya washtakiwa hao ilishabadilishwa na kwamba hati ya sasa haineshi kiwango cha pesa au hasara iliyosabibishwa.

Baada ya kusikilizwa kwa hoja za pande zote Jaji Mkuu aliahirisha kesi hiyo

No comments:

Post a Comment