KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Jaji Kaganda kuwashughulikia viongozi wasiotaja mali zao


Leon Bahati na Eveline Kijumbe
KAMISHINA mpya wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda ameanza kazi kwa kuahidi kula sahani moja na viongozi wa umma ambao wataficha au kutotaja mali wanazomiliki. Jaji Kaganda alisema kama kuna viongozi waliotumia mwanya wa baadhi ya mapungu katika usimamizi wa sekretarieti hiyo miaka iliyopita, sasa wajue watakumbana na msumeno wa sheria. “Inawezekana kulikuwepo na mapungufu (kwenye uongozi wa sekretarieti) miaka iliyopita, lakini mimi nitajitahidi nisiingie kwenye mapungufu hayo,” alisema Kaganda katika mahojiano na waandishi wa habari jana.

Alikuwa akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu mikakati yake mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam, jana. Maswali ya waandishi wengi yaliegemea zaidi katika kujua jinsi atakavyokabiliana na viongozi amboa wamekuwa wakificha baadhi ya mali zao, kinyume na taratibu za nchi na udhaifu wa uongozi wa sekretarieti hiyo kushughulikia wanaoficha mali zao.

Kaganda alisema kwamba Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayowataka wataje mali zao iko wazi, hivyo atajitahidi katika uongozi wake kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa kikamilifu. Katika maelezo yake, Kaganda alikuwa akikwepa kuonekana dhahiri kukubali shutuma dhidi ya viongozi waliopita wa sekretarieti hiyo. Badala yake, alielezea kuwa ni mapungufu ya kawaida ambayo yanaweza kujitokeza kwa uongozi wowote hivyo akasema kwamba atajitahidi kuhakikisha kuwa udhaifu wa namna hiyo haujitokezi.

“Mimi siwezi kusema kwamba kulikuwa na uzembe katika uongozi uliopita. Lakini inawezekana kulikuwa na mapungufu. Nitajitahidi nisiingie kwenye mapungufu hayo,” alisema Kaganda ambaye aliandamana na familia yake katika hafla hiyo fupi ya kuapishwa. Sekretarieti hiyo imekuwa ikilaumiwa kwa kutofanya kazi kwa uwazi na hivyo kusababisha viongozi wengi wa kisiasa kutumia mwanya huo kutotangaza mali zao halisi.

Lawama za namna hiyo zimekuwa zikielekezwa kwenye taasisi hiyo kutokana na imani kuwa viongozi wamekuwa wakijilimbikizia mali wanazopata kinyume cha sheria. Kamishna huyo alisisitiza kwa kuwa sheria ya kutaja mali iko wazi, katika uongozi wake hakuna atakayekwepa kutekeleza sheria hiyo. “Kuandikisha mali zote unazomiliki ni sehemu ya uongozi wa umma na hii inaenda kwa kiapo. Tutafuatilia ili kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo,” alisema. Miongoni mwa viongozi wanaowajibika kwenye sheria hiyo ya maadili ni rais, mawaziri, wabunge pamoja na viongozi wengine ambao wanateuliwa na rais kwa mujibu wa katiba.

Jaji Kaganda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Stephen Ihema ambaye amemaliza muda wake. Kabla ya kustaafu, Kaganda alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kusini. Wakati huo huo, Rais Kikwete jana aliwapokea mabalozi wapya wawili ambao ni Pierluigi Velardi wa Italia na Alexander Rannikh wa Russia

No comments:

Post a Comment