KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 12, 2010

Watuhumiwa ugaidi Uganda: Tulihusika

Wapelelezi nchini Uganda wamewakamata watu wanne ambao wanasema walipanga mashambulio ya mabomu yaliyowauwa watu 70 mnamo mwezi uliopita.

Watu hao walikiri kuhusika kwao katika mashambulio hayo wakati wa mkutano na waandishi habari siku ya Alhamisi mjini Kampala.

Wote walizungumzia mchango wao katika mashambulio hayo dhidi ya klabu ya raga na mkahawa mmoja.

Maeneo yote mawili yalikuwa na mashabiki wa waliokuwa wakiangalia fainali ya kandanda ya Kombe la Dunia.

Watuhumiwa hao wanne walifikishwa kwenye mkutano na waandishi wa habari uliotayarishwa na serikali ya Uganda.

Wapelelezi katika nchi za Uganda na Kenya wamekwishawazuia watu kadhaa inaoaminiwa walihusika na mashambulio hayo.
Majeshi kujiamini

Lakini hii ni mara ya kwanza kwa vikosi vya usalama nchini Uganda kusema wamewagundua watu waliopanga njama ya mashambulio hayo.

Watuhumiwa hao waliwaambia wanahabari kwamba walipanga mashambulio hayo kutokana na imani yao ya kidini.

Mara tu baada ya mashambulio hayo kundi la wanaharakati wa siasa kali za Kiislamu nchini Somalia, al-Shabab lilisema lilihusika.

Lilisema mashambulio hayo yalifanywa kulipiza kisasi kwa kitendo cha Uganda kutuma wanajeshi wake nchini Somalia kama sehemu ya vikosi vya Muungano wa Afrika vya kulinda amani, vilivyopelekwa kusaidia serikali iliyoelemewa nchini humo.

Katika mkutano huo na wanahabari mjini Kampala, mmoja wa watuhumiwa alisema yeye ni kiungo cha mawasiliano na al-Shabab.

No comments:

Post a Comment