KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, August 10, 2010

Wakala wa Campbell atoa ushahidi tena


Wakala wa zamani wa mwanamitindo maarufu Naomi Campbell amerejea tena kutoa ushahidi wake katika kesi inayoendelea inayomhusu aliyekuwa rais wa Liberia Bw Charles Taylor.

Carole White aliiambia mahakama Jumatatu kuwa Taylor alimpa Bi Campbell almasi baada ya chakula cha jioni Afrika Kusini mwaka 1997.

Ushahidi wake unapingana na wa Bi Campbell alipoiambia mahakama kuwa hakujua almasi hizo zilitoka kwa nani.

Bw Taylor anashtakiwa kwa kuwapa silaha waasi wa Sierra Leone kwa kubadilishana na almasi.

Maelfu ya watu walikufa kutokana na migogoro inayohusishwa na waasi hao nchini Sierra Leone na Liberia katika miaka ya 80 na 90.

Bw Taylor anakabiliwa na mashtaka 11 yanayohusishwa na migogoro katika mahakama maalum ya Sierra Leone inayosikiliza kesi hiyo mjini The Hague.

Waendesha mashtaka wanajaribu kumhusisha kiongozi huyo wa zamani wa Liberia na almasi ambazo Bi Campbell alipokea. Amekana kuhusika kwa namna yeyote na biashara iliyopewa jina la almasi zilizotumika kugharamia vita.

Zawadi ya usiku

Kwa mujibu wa ushahidi wa Bi White, Taylor na Bi Campbell tayari walikuwa na dalili za mahusiano ya kimapenzi wakati wa chakula cha jioni mwaka 1997 kilichoandaliwa na Nelson Mandela, Rais wa Afrika Kusini wakati huo.

Bw Taylor alimwambia mwanamitindo huyo wakati wa chakula cha jioni kuwa angemtumia watu kumpelekea almasi, Bi White aliiambia mahakama.

Alisema Bi Campbell alikuwa anawasiliana na wale watu na alikuwa ‘mwenye furaha’ kuhusu almasi hizo.

Mwigizaji wa Kimarekani Mia Farrow, aliyehudhuria pia chakula hicho cha jioni, alitoa ushahidi wake Jumatatu kwamba Bi Campbell alifurahia zawadi hiyo.

Wiki iliyopita Bi Campbell aliiambia mahakama kuwa watu wawili walikuja chumbani kwake usiku na kumpa kifuko cha mawe na kwamba hakujua nani aliyempa zawadi hiyo.

Courtenay Griffiths, wakili anayemtetea Charles Taylor alisema Bi White alikuwa na ‘sababu zake binafsi’ za kudaganya kwa sababu ya kuvunjika kwa mkataba kati yake na Bi Campbell. Alihoji pia uwezo wa Bi White kukumbuka mambo na kutokuwa na upendeleo.

Bw Taylor, 62, alikamatwa mwaka 2006 na kufunguliwa mashataka mwaka 2007.

Kiongozi huyo wa kivita wa zamani anatuhumiwa kuwapa silaha waasi wa Sierra Leone wa Revolutionary United Front (RUF) wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1991 na 2002, madai ambayo ameyakanusha.

Waendesha mashtaka wanasema kwa kutumia mamlaka yake huko Liberia Bw Taylor pia alitoa mafunzo na kuamuru waasi kuua, kubaka na kuwatesa raia wa Liberia, mara kwa mara wakiwakata mikono na miguu.

Vita nchini Sierra Leone ilisambaa zaidi kwa kutumia askari watoto.

Kesi ya Bw Taylor ilipata mwamko hafifu wa vyombo vya habari vya kimataifa mpaka hapo Bi Campbell alipotoa ushahidi wake.

No comments:

Post a Comment