KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, August 10, 2010

Mbunge wa Zambia aliyefungwa alalamika


Mbunge mmoja wa Zambia aliyefungwa gerezani kwa siku 60 amelalamika kuwa wafungwa nchini humo hawapewi kifungua kinywa.

George Mpombo, aliyekuwa waziri wa ulinzi, aliyasema hayo alipohukumiwa kwa kutoa hundi akitaka pesa kwenye akaunti ya benki ambayo haina kiwango cha kutosha kulingana na hundi hiyo.

Hivi karibuni alijiuzulu kwenye wadhifa wake wa ulinzi baada ya hundi yake yenye thamani ya dola za kimarekani 2000 kukataliwa Desemba iliyopita.

Bw Mpombo, ambaye anakata rufaa dhidi ya shtaka hilo, alisema hali halisi katika magereza ya Zambia ni ya "karaha".

Mahakama huko Ndola, katika jimbo la Copperbelt, pia imemtoza faini ya dola za kimarekani 800 siku ya Jumatatu.

Hakimu Kelvin Limbani alisema kesi kama hizo zilikuwa na athari kubwa, zinazodhuru uchumi wa nchi, na hukumu yake itakuwa kama mfano.

Gazeti la Zambia la Lusaka Times lilimnukuu Bw Limbani akisema, " Unastahili kuadhibiwa ili uweze kujirekebisha na kwa wanaotaka kufanya uhalifu waweze kujizuia kufanya kosa kama lako."

Akizungumza akiwa kifungoni baada ya kuhukumiwa, Bw Mpombo aliwaambia waandishi wa habari kwamba alitaka kukata rufaa kwa tume ya kutetea haki za binadamu ya Zambia ili kutafuta suluhu ya magereza yaliyojaza watu kupita kiasi.

Bw Mpombo, anayewakilisha jimbo la Kafulafuta kupitia chama cha Movement for Multiparty Democracy, amekuwa waziri kwa miaka kadhaa.

Ameshatumika chini ya uongozi wa marehemu Rais Levy Mwanawasa, pamoja na mrithi wake Rupia Banda.

Mwandishi wa BBC nchini humo Mutuna Chanda aliyopo mji mkuu wa Lusaka, alisema Bw Mpombo amekuwa mkosoaji wa Bw Banda tangu alipojiuzulu kwenye baraza la mawaziri.

No comments:

Post a Comment