KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, July 20, 2010

Mlevi Ampanda Mamba Mgongoni


Mwanaume mmoja wa nchini Australia aliyekuwa amelewa chakari amelazwa hospitali baada ya kujeruhiwa na mamba alipoamua kumfanya mamba kama farasi kwa kumdandia mgongoni.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 36 alifukuzwa baa baada ya kuonekana pombe zimemzidia ndipo alipoamua kwenda kwenye bustani ya wanyama ya mjini Broome nchini Australia.

Mwanaume huyo aliipanda fensi na kuingia kwenye bustani hiyo kabla ya kujisogeza kwenye sehemu ambayo wametengewa mamba.

Katika tukio hilo lililotokea kwenye majira ya saa nne usiku, mwanaume huyo alimsogelea mamba mwenye urefu wa mita 2.8 na kujaribu kumnyeshwa bia kabla ya kuamua kurukia kwenye mgongo wa mamba huyo aliyepewa jina la Fatso.

"Alitoka kwenye eneo hilo na kwenda kwenye eneo jingine ambalo lilikuwa na mamba mwenye urefu wa mita 5", alisema msemaji wa polisi na kuongeza "Aliona ni wazo zuri kukaa juu ya mamba huyo aendeshwe kama farasi".

"Mamba alijipindua na kuung'ata mguu wake", alisema msemaji huyo wa polisi.

Alifanikiwa kuchoropoka akiwa amejeruhiwa vibaya sana, aliwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi.

"Ana bahati sana kuwa hai hadi leo, mtu mwenye akili timamu hawezi kukaa juu ya mamba mwenye urefu wa mita 5", alisema afisa mwingine wa polisi.

Taarifa zinasema kuwa mmiliki wa bustani hiyo hana mpango wa kumfungulia mashtaka mwanaume huyo.

No comments:

Post a Comment