KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 9, 2010

Hitilafu yaukumba mkongo wa A Mashariki


Mkongo wa mawasiliano ukiwekwa mjini Mombasa, Kenya Juni 2009

Mkongo wa mawasiliano uliopitishwa chini ya bahari kwa nia ya kuongeza kasi kwa watumiaji wa tovuti Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza umepata hitilafu, na kusababisha wengi katika eneo hilo kukosa huduma hiyo.

Wamiliki wa kampuni ya Seacom wamesema sababu hasa ya hitilafu hiyo "bado inafanyiwa uchunguzi", lakini inadhaniwa chanzo chake kimeanzia katika pwani ya Kenya.

Mkongo huo, uliokamilika mwaka 2009, unaunganisha Afrika Kusini, Tanzania, Kenya, Uganda na Msumbiji hadi Ulaya na Asia.

Seacom imesema "imeandaa ukarabati wa dharura", ambao huenda ukafanyika kwa siku nane.

Katika taarifa iliyotoa ilisema, " Hitilafu hiyo iliyotokea bila kutarajiwa inaathiri usafirishaji wa mawasiliano ya intaneti kote India na Ulaya. Usafirishaji wa huduma hiyo ndani ya Afrika haujaathirika."
Muda usiotabirika

Kampuni hiyo ilisema imekuwa ikishughulikia tatizo hilo tangu iliporipotiwa kwa mara ya kwanza tarehe 5 Julai ili kutafuta njia mbadala za kusafirisha mawasilaiano ya intaneti , ikiwemo kutumia mkongo mbadala.

" Suluhu za kurejesha huduma hizo kwa sasa zinafanyiwa kazi."

Mkongo huo wa mawasiliano ulipokamilika Julai 2009, kampuni hiyo iliahidi kupunguza gharama za kuunganisha huduma za tovuti na kuimarisha uwezo wake katika eneo hilo.

Hata hivyo, wataalamu wanasema gharama bado ni kubwa kwa wengi wanaoishi eneo hilo.

Tatizo hilo limewaathiri zaidi wanaotumia huduma hiyo nyumbani, kwani biashara nyingi eneo hilo walijiandaa kwa njia mbadala iwapo kutatokea hitilafu.

Ni hitilafu kubwa ya pili kutokea tangu mkongo huo ulipoanza shughuli zake rasmi.

Makosa kama haya hutokea katika kipindi maalum. Mkongo uliosimamishwa huko Mediterranean mwaka 2008 ulivuruga kwa muda usafirishaji wa mawasiliano ya intaneti kufikia asilimia 70 huko Misri na asilimia 60 India.

Kampuni hiyo ilisema meli moja itapelekwa ili kurekebisha mkongo huo.

" Muda halisi wa kukarabati hautabiriki kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao kama vile muda wa kufika meli hiyo, hali ya hewa na muda wa kutambua ulipo mkongo huo. Kutokana na sababu hizo, makadirio ya muda wa kukarabati unbaki kuwa na utata."

Taarifa hii imetolewa, huku mkongo mwengine unaounganisha Afrika na Ulaya ukiwa umezinduliwa.

Mkongo huo mkuu unaunganisha Ulaya ya magharibi, Ghana na Nigeria.

No comments:

Post a Comment