KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 9, 2010

Ghana yataka FIFA ibadili sheria


Waziri wa michezo wa Ghana amesema shirikisho la soka duniani FIFA linatakiwa kubadilisha sheria za mchezo wa soka kufuatia kuondolewa kwa Ghana kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kutumika mikono.

Waziri huyo Akua Sena Dansua hajasema ni sheria zipi angetaka zibadilishwe, lakini watu wengi wamekuwa wakisema mwamuzi wa mchuano wa robo fainali kati ya Ghana na Uruguay angetakiwa kuipa Ghana goli, wakati mchezaji wa Uruguay Luis Suarez alipoondosha kwa mikono mpira uliokuwa unaingia kwenye lango la timu yake.

Kwenye mechi hiyo mshambuliaji wa Ghana Dominic Adiyah alipiga mpira kwa kichwa ukaeleka kuingia katika lango la Uruguay ukibakia muda mfupi sana kabla ya mechi kumalizika, lakini Suarez ambaye ni mchezaji wa ndani akauondosha kwa mikono.

Mwamuzi alimwonyesha kadi nyekundu Suarez na akawapa Ghana penati ambayo Asamoah Gyan alipiga nje.

Adhabu hiyo ni kulingana na sheria zilizopo za shirikisho la soka dunia FIFA.

Mechi ilimalizika kwa sare, ikalazimika kuingia mikwaju ya penalti na Uruguay wakaibuka washindi wa mabao 4-2.

Ghana ilikuwa timu ya Afrika kufikia hatua ya robo fainali katika Kombe la Dunia.

Baada ya kurejea nyumbani Black Stars walipokelewa kwa shangwe na nderemo mjini Accra.

Rais wa Ghana John Atta Mills alisema wachezaji hao watapewa tuzo za kitaifa na pia dola 20,000 kila mmoja.

Mashabiki wa soka kote barani Afrika waliishabikia Ghana wakati wa mchuano huo, na wengi walipigika sana baada ya Black Stars kuondolewa.

Ilikuwa ni timu pekee ya Afrika iliyobakia kwenye mashindano baada ya timu zingine tano za Afrika kuondolewa kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment