KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, July 9, 2010

Fainali ni Uhispania na Uholanzi


Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini itakuwa kati ya Uhispania na Uholanzi.

Uhispania imeishinda Ujerumani bao 1-0 katika uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban na kufuzu fainali kwa mara ya kwanza.

Bao la Uhispania lilifungwa kwa kichwa na mlinzi Carles Puyol katika dakika ya 73, kufuatia mpira wa kona.

Ujerumani walionekana kikosi tofauti kabisa na timu ambayo iliiondoa England kwa kuifunga mabao 4-1 na baadaye ikaiondoa Argentina kwa kuifunga mabao 4-0.
Muller akosekana

Pengo la mshambuliaji Thomas Muller ambaye alikuwa nje kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano lilikuwa wazi kabisa kwenye safu ya ushambuliaji ya Ujerumani.

Muller ambaye ameshafunga mabao manne kwenye Kombe la Dunia alipata kadi ya pili ya njano kwenye mechi kati ya Ujerumani na Argentina, na bila yeye, kocha Joachim Loew alikosa kabisa mbinu za ushambuliaji kwa timu ya Ujerumani.

Uhispania walidhibiti mchezo katika muda wote, na wangeweza kufunga mabao mengi zaidi lakini umaliziaji ukawa mbaya, pamoja na mlinda lango wa Ujerumani Manuel Nuer kuokoa sana.

Fainali ya siku ya Jumapili kati ya Uhispania na Uholanzi katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg itawakutanisha wafungaji wanaaongoza ; Wesley Snijder na David Villa.

Ni mara ya kwanza kwa Uhispania kucheza fainali ya Kombe la Dunia,na kwa upande wa Uholanzi itakuwa mara ya tatu, ingawa bado hawajapata kushinda Kombe hilo.

Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na wanne itachezwa Jumamosi kati ya Uruguay na Ujerumani.

No comments:

Post a Comment