KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 17, 2010

Clinton, Hague wajadili suala la Lockerbie


Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, amezungumza na Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, William Hague, kuhusu hatua ya kuachiliwa mapema mwaka jana kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kulipua ndege ya Marekani mjini Lockerbie, Abdelbaset al-Megrahi.


Katika mazungumzo ya simu, mawaziri hao wawili walikubaliana kuwa uamuzi wa kuachiliwa kwa al-Megrahi kutoka jela ya Scotland na kumpeleka Libya ulikuwa ni makosa.

Bi Clinton alisema Uingereza huenda ikatoa maelezo ya moja kwa moja katika baraza la Congress kuhusu kuachiliwa huru kwa Bw Megrahi.

Uamuzi wa kumwachia huru al-Megrahi ulichukuliwa kutokana na sababu za kiafya na serikali ya Scotland.

Baraza la senate la Marekani mwezi huu litajadili suala hilo, kufuatia tuhuma kuwa shirika la BP la nchini Uingereza lilichangia katika uamuzi huo ili liweze kupatiwa kandarasi kubwa nchini Libya.

Lakini BP, serikali za Uingereza na Libya zinakanusha madai hayo.

Al-Megrahi aliachiliwa huru mwezi August mwaka uliopita na Waziri wa Sheria wa Scotland kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na saratani, na wakati huo ilisemekana hatoweza kuishi zaidi ya miezi mitatu.

Marekani inasema kuna masuali ambayo yanapaswa kujibiwa kuhusu maelezo ya afya yaliyosababisha kuachiliwa huru kwa Bw Megrahi.

Alihukumiwa kifungo cha maisha mwaka wa 2001 kutokana na kulipuliwa kwa ndege mjini Lockerbie, ambayo iliwauwa watu 270 wengi wao wakiwa raia wa Marekani.

Karibu mwaka moja sasa anaendelea kuishi, hali ambayo ilizusha hasira miongoni mwa makundi yanayowatetea waathiriwa wa mkasa huo.

No comments:

Post a Comment