KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 3, 2010

Brazil yaondolewa na Uholanzi


Mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, Brazil, wameondolewa kwenye michuano ya mwaka huu baada ya kuzidiwa maarifa na kuchapwa mabao 2-1 na Uholanzi, katika mechi ya robo fainali iliyopigwa uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port Elizabeth.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Brazil wakiongoza bao 1-0, lililofungwa katika dakika ya 10 na Robinho, lakini kwenye dakika ya 53 mlinzi Felipe Melo alijifunga na kuwapa Uholanzi bao la kusawazisha, na baadaye akazidi kuandamwa na mkosi akaonyeshwa kadi nyekundu.

Bao la ushindi la Uholanzi lilifungwa kwa kichwa na Wesley Sneijder katika dakika ya 68 kumalizia mpira wa kona.

Kona hiyo ilitokana na mlinzi Juan kuutoa nje mpira pasipo ulazima akiwa hajaandamwa na wachezaji wa Uholanzi, na ni miongoni mwa makosa ambayo Brazil itaendelea kujutia.

Felipe Melo alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga Arjen Roben akiwa chini.

Kwa ushindi huo, Uholanzi wamelipiza kuondolewa mara mbili na Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 na 1998.
Nusu fainali

Uholanzi wanasubiri kuchuana kwenye nusu fainali na mshindi kati ya Ghana na Uruguay siku ya Jumanne.

Hata hivyo watakuwa bila mlinzi Gregory van der Wiel na kiungo Nigel de Jong ambao wote wawili wana kadi mbili za njano.

Katika dakika ya nane Robinho alifunga bao, lakini bendera ya msaidizi wa mwamuzi ikawa imenyanyuka kuashiria aliotea.

Hazikupita zaidi ya dakika mbili tena kabla ya Robinho kuipenya tena ngome ya Waholanzi na kuipatia Brazil bao la kuongoza.

Baada ya Uholanzi kufunga bao la pili na Melo kuonyeshwa kadi nyekundu Brazil walififia kimchezo, kiasi kwamba Uholanzi walitishia kufunga mara kwa mara huku wakiwadhibiti washambuliaji wa Brazil.

Jedwali hapo chini linaonyesha jinsi mechi ilivyochezwa.
This content requires Flash Player version 10 (installed version: No Flash Flayer installed, or version is pre 6.0.0)

No comments:

Post a Comment