KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, June 17, 2010

..Waasi wa Darfur wajisalimisha Hague


Viongozi wawili wa waasi Darfur wamejisalimisha katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC iliyopo mjini Hague.

Waasi hao, Abdallah Banda Abakaer Nourain na Saleh Mohammed Jerbo Jamus, walishtakiwa kisiri mwaka jana.

Wanatakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita wakihusishwa na vifo vya wanajeshi wa kutunza amani 12 wa Umoja wa Afrika, AU mwaka 2007.

Mapema mwaka huu, mashtaka dhidi ya kiongozi mwengine muasi aliyehusishwa na shambulio hilo hilo yalifutiliwa mbali kutokana na kukosa ushahidi wa kutosha.

Majaji wa ICC walitoa uamuzi kuwa waendesha mashtaka hawakuweza kuthibitisha Bahr Idriss Abu Garda, ambaye pia alijisalimisha, alipanga shambulio hilo katika kambi ya AU Septemba 2007.

Mashtaka
Katika taarifa yake, ICC imesema washukiwa hao wawili watakabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu wa kivita watakapofikishwa mahakamani siku ya Alhamis ikiwa ni pamoja na mauaji, kuwashambulia makususdi wanajeshi wa kutunza amani moja kwa moja na wizi wa mali.

Inadaiwa washambuliaji hao, takriban 1,000, walikuwa na makombora ya kudungulia ndege, mizinga na maguruneti.

Kuanzia Januari 2008, Umoja wa Mataifa ulianza kudhibiti muungano wa jeshi hilo la kutunza amani mjini Darfur ukiwa na idadi kubwa zaidi na mamlaka ya juu zaidi.

Mwaka jana, Rais wa Sudan Omar al-Bashir alishtakiwa kuhusika na uhalifu wa kivita, shtaka la mwanzo kutolewa na ICC dhidi ya Rais aliye madarakani.

Amekana vikali kuhusika na mashtaka hayo, na serikali yake imesema takwimu za watu waliofariki dunia katika mgogoro wa Darfur zimetiwa chumvi.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 300,000 wameuawa Darfur na zaidi ya watu milioni 2.6 wamehama makazi yao tangu waasi waanze mapigano mwaka 2003.

Waziri mmoja wa serikali hiyo pamoja na kiongozi wa kijeshi anayeunga mkono serikali nao wameshtakiwa kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita Darfur.

No comments:

Post a Comment