KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, June 18, 2010

Umeishajitolea Kuchagia Damu?


Wakazi wa jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine ya Tanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangia mpango wa damu salama ili kuokoa na kuzuia vifo vya akina mama wajawazito, watoto na wahanga wa ajali.
Hayo yalisemwa na Meneja wa mpango wa damu salama Kanda ya Mashariki, Grace Mlingi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya uchangiaji wa damu salama katika viwanja vya Biafra ambapo baadhi ya wananchi na wanafunzi wa sekondari walijitokeza kwa wingi kuchangia damu.

Kilele cha maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu kitaifa kinatarajia kufanyika jijini Mwanza kwenye Viwanja vya Gand.

Mlingi aliwaomba wananchi waendelee kujitokeza kuchangia damu bila kuogopa ili kuokoa wananchi wote wanaohitaji damu pindi wapatapo matatizo yakiwemo ya pindi akinamama wanaojifungua, ajali na watoto.

Aliendelea kusema kuwa, mpaka sasa kunahitajika uniti nyingi za damu ili kukidhi mahitaji ya nchi.

“Nchi inahitaji Uniti za damu salama lita laki tatu na nusu, lakini hazitoshi, hivyo malengo yetu ni kuhakikisha tunakusanya lita 100 kwa siku.”

Kwa upande wake Afisa viwango kanda ya mashariki, Ndeunasia Towo alisema kuwa wataendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kukidhi mahitaji kwa walengwa.

“Mpaka sasa tunaendelea kuhamasisha klabu za wachangia damu ambazo nyingi zimeundwa mashuleni na nyingine ni za watu binafsi” alisema Towo.

Katika uchangiaji huo ambao ulianza tokea Juni Mosi tayari wameishakusanya damu lita 300, huku wakiendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia.

Wananchi wametakiwa kuondoa hofu zao na kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wenye kuhitaji damu.

No comments:

Post a Comment