KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, June 18, 2010

Radi Yawatenganisha Kabla Hawajachumbiana


Mwanaume mmoja wa nchini Marekani alipanga kumfanyia suprise na kumvalisha pete ya uchumba mpenzi wake juu ya mlima lakini wakiwa nusu ya safari walipigwa na radi na mpenzi wake alifariki hapo hapo.
Richard Butler, 31, wa Knoxville, Tennessee nchini Marekani alimchukua mpenzi wake Bethany Lott na kumpeleka kwenye mlima wa Max Patch Bald uliopo North Carolina.

Richard anasema kuwa alitaka mpenzi wake huyo ambaye ana umri wa miaka 25 afikirie wapo kwenye tripu ya kupanda mlima wakati lengo lake kuu lilikuwa ni kumpigia goti kuomba akubali kuolewa naye na kumvalisha pete ya uchumba ambayo aliificha kwenye mfuko wake wa suruali.

Mvua kubwa zilizoanza kunyesha ghafla hazikuwazuia wapenzi hao kuendelea na safari yao, lakini hali ya hewa ilizidi kuwa mbaya na miungurumo ya radi ilianza kusikika.

Radi tatu zilipiga eneo walilokuwepo na mojawapo ya radi hizo iliwatandika wapenzi hao na kuwarusha mita kadhaa chini.

"Umeiona hiyo?", alisema Richard ambaye wakati huo hakujitambua kuwa ameungua robo tatu ya mwili wake.

Mpenzi wake hakujibu kitu hali iliyomfanya Richard awahi sehemu aliyodondokea kujua kulikoni.

Richard alijaribu kumpa huduma ya kwanza mpenzi wake ambaye alizimia baada ya kupigwa na radi.

Madaktari waliowasili eneo la tukio, walijaribu kila njia kumzindua Bethany kwa muda wa lisaa limoja kabla ya kumpa taarifa Richard kuwa Bethany amefariki.

No comments:

Post a Comment