KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, June 21, 2010

Algeria yaibana England


England na Algeria zilitoka sare 0-0 siku ya Ijumaa katika mechi ya kundi la C kwenye michuano ya Kombe la Dunia mjini Cape Town, matokeo yaliyoiweka England katika hatari ya kuyaaga mashindano mapema kuliko ilivyotarajiwa.


Wayne Rooney akidhibitiwa vilivyo na wachezaji wa Algeria.

Ili kufuzu kwa raundi ya pili ni lazima England ipate ushindi mkubwa katika mechi inayofuata dhidi ya Slovenia, ambayo ilitoka sare na Marekani 2-2.

Slovenia sasa inaongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi 4 kutokana na mechi 2, baada ya kuishindia Algeria 1-0 katika mechi ya kwanza, na baada ya kutoka sare 2-2 na Marekani.

Marekani ina pointi mbili sawa na england lakini Marekani iko mbele kwa wingi wa mabao; nayo Algeria ina pointi moja kutokana na sare ya Ijumaa.

Wachezaji wa England walizomewa na mashabiki wao baada ya mechi hiyo iliyodhibitiwa zaidi na Algeria.

Mabadiliko
Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney, alionekana mdhaifu muda wote wa mechi hiyo ingawa kocha Fabio Capello alifanya mabadiliko kuwaondoa Emile Heskey, Gareth Barry na Aaron Lennon ambao nafasi zao zilichukuliwa na Shaun Wright-Philips, Jermain Defoe na Peter Crouch.

Kutokana na mabadiliko hayo Jermain Defoe aliisumbua mara kadhaa safu ya ulinzi ya Algeria lakini bila mafanikio ya kutikisa nyavu.

Capello alikuwa amempumzisha mlinda lango Robert Green ambaye katika mechi ya kwanza alilaumiwa kwa kosa lililoipa Marekani bao la kusawazisha,na nafasi hiyo kuchukuliwa na David James.

Kocha wa Algeria Rabah Saadane naye pia alimpumzisha kipa Fawzi Chaouchi ambaye vile vile alifanya kosa katika mechi ya ufunguzi lililowapa ushindi Slovenia na kumchezesha Rais M'Bolhi.

Wasi wasi
Rooney alitazamiwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, lakini katika mchezo wa Ijumaa wazo hilo lilionekana kama dhana isiyokubalika.

Badala ya Rooney, kiungo wa Algeria Karim Ziani anayeichezea klabu ya Wolfsburg ndiye aliyeonekana kutia fora zaidi.

Mlinzi Jamie Carragher alipata kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea visivyo Hassan Yebda, na atakosa mechi inayofuata

No comments:

Post a Comment