KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, May 15, 2010

Wazazi wadaiwa kulipa fedha nyingi kuwakomboa


Utapeli wa kutisha umeingia mkoani Kilimanjaro, ambapo mtu mmoja (jina tunalihifadhi) ameiba mtoto wa kiume anayesoma darasa la pili, mwenye umri wa miaka minane na kumtoroshea jijini Kampala, Uganda.

Mwanafunzi huyo jina linahifadhiwa alikuwa anasoma katika shule ya msingi Korongoni Manispaa ya Moshi.

Baada ya kumtoroshea Uganda, mtu huyo aliwadai wazazi wa mtoto huyo dola za Marekani 1,000 ili wamrejeshe mtoto huyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa kuelezea utapeli huo na namna walivyompata mtoto wao, baba wa mtoto huyo, mkazi wa Oysterbay na mfanyabiashara wa soko la Mbuyuni mjini hapa, alisema kuwa mwanaye alipotea tangu Aprili 18, mwaka huu.

Mzazi huyo alisema siku ya tukio walirejea nyumbani kutoka shambani eneo la Punguani wilayani Moshi Vijijini majira ya saa moja jioni lakini hawakumkuta mtoto wao hivyo wakaanza kumtafuta.

Alisema baada ya kumkosa kwa ndugu, jamaa na marafiki, walikwenda kituo kikuu cha Polisi mjini hapa na kutoa taarifa.

Baada ya kutoa taarifa, waliambiwa kuwa zikipita saa 24 bila mtoto huyo kuonekana polisi wangeaza uchunguzi. Mzazi huyo alisema baada ya kupita siku 17, polisi waliwajulisha kuwa kuna mtoto amepatikana na kwamba alikuwa kituo cha polisi cha Majengo mjini hapa.

Kwa mujibu wa baba mzazi huyo, walimuona mtoto husika, lakini hakuwa wa kwao.

Alisema baada ya wiki moja kupita tangu waelezwe habari za mtoto aliyekuwa Majengo, wakala wa basi la Kampala Coach namba UAL 248H, alidai kuwa alipigiwa simu na mtu mmoja kutoka Uganda ambaye alimwelekeza awasiliane nao ili awape mawasiliano kwa lengo la kuwasiliana na mtu aliyemchukua mtoto wao.

Alisema ndugu waliwasiliana na mtu huyo kwa namba 01405915501 ambaye alidai kuwa yuko Uganda na kwamba anahitaji kiasi hicho cha fedha ndipo amuachie mtoto huyo na akawapa muda wa siku tatu kuwasilisha fedha hizo vinginevyo atamuuza mtoto huyo.

Mzazi huyo alisema kuwa alirudi polisi na kuwaomba msaada, lakini walimwambia kuwa hawawezi kumsadia kwani hawana uwezo wa kusafirisha polisi hadi nje ya nchi na kwamba kibali cha kusafirisha polisi husika ni lazima kitoka makao mkuu Dar es Salaam.

Alisema majibu hayo hayakumridhisha na kuamua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Musa Samizi, ambaye aliwajibu kuwa yeye ni mwanasiasa na suala hilo ni la kipolisi zaidi na kuwashauri warudi polisi ili kupata msaada.

Alisema baada ya kurudi polisi waliwaomba wawape barua ili watakapokuwa Uganda wasipate matatizo yoyote hivyo, polisi wakawapa barua.

Alisema kuwa waliwasiliana na mtu huyo na kumuomba apunguze kiwango, na kuwakubalia wampe dola 400 na baada ya kukubaliana, aliwapa masharti ya kuzibadili fedha hizo kutoka Shilingi ya Tanzania na kuwa Dola.

Alisema walianza mchakato wa kutafuta pasi za kusafiria na kwamba wafanyabiashara wenzake walimchangia Sh. million 1.5 kwa ajili ya nauli, malazi na kumlipa mtu huyo.

Alisema walianza safari Mei 12, mwaka huu, yeye na mtu mmoja aliyeteuliwa na wenzake jina tunahifadhi na kuanza safari hadi mji wa Busia mpakani mwa Kenya na Uganda.

Mtu aliyechukua mtoto wake alikuwa amewapa maelekezo kwamba washuke hapo. “Baada ya kufika alituambia twende kwenye benki ya Stanbic eneo la Jinja na tuweke fedha tutampata mtoto. Tuliweka fedha kwenye akaunti namba 0140592455501 Mei 13, tulikaa kwa saa sita tukisubiri na tulianza kuwa na hofu kuwa tumepoteza fedha, lakini alitupigia akidai anatuona hapo benki,” alisema na kuongeza:

“Alitupa namba ya ambaye atamleta mtoto.”

Alisema baada ya muda simu haikupatikana tena, lakini baada ya muda walipokea simu kutoka kwa ndugu zao Moshi, ambao mtu huyo alikuwa akiwasiliana nao na kuwaambia wawaambie waende kituo cha daladala watamkuta mtoto wao na baada ya kufika daladala waliwasiliana na kondakta ambaye alimpeleka mtoto akiwa na mfuko wenye nguo zake.

Mzazi huyo alisema walishindwa kuchukua hatua zozote kwa kuwa kondakta huyo alidai kuwa alipewa mtoto huyo amshushe kwenye kituo hicho apokelewe na wazazi wake.

Akizungumzia tukio hilo, mtoto huyo alisema alichukuliwa na mtu huyo nyumbani kwao na kumwabia anakwenda kumnunulia mhindi, na kwamba alimsafirisha kwa gari na alimfikisha Uganda.

Mtoto huyo alisimulia kuwa alikuwa anapewa kila kitu katika nyumba aliyokuwa anaishi na kwamba amewaacha wenzake watatu.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO), Linus Sinzumwa, alisema kuwa wazazi wa mtoto huyo walishindwa kuwa na subira kwani waliambiwa wasubiri mawasiliano kati ya Polisi wa Tanzania na Polisi wa kimataifa (Interpol).

Alisema baba wa mtoto alitoa taarifa Mei 4 na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi.

Sinzumwa alisema wameshapata namba ya mtu aliyemtorosha mtoto huyo, hivyo wanashirikiana na Interpol kumtia mbaroni.

Polisi waliokwenda eneo la tukio kwa ajili ya kumchukua mtoto huyo na wazazi wake, wananchi waliwagomea na kuwafukuza kwa kusema kuwa walikosa msaada wa polisi na walijichangisha wenyewe na kufanikisha kupatikana kwa mtoto huyo.

Hata hivyo wananchi wa eneo la Mbuyuni waliandamana kumpokea mtoto huyo na wazazi wake katika kituo cha mabasi mjini hapa na kuzunguka kwa maandamano hadi nyumbani kwao.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wananchi walisema ni uzembe wa polisi kwani wangeonyesha jitihada wangeokoa fedha hizo na kumkamata aliyemtorosha mtoto huyo.

No comments:

Post a Comment