KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, May 21, 2010

Villa ajiunga na Barcelona


David Villa atatambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Barcelona siku ya Ijumaa, baada ya kukamilisha taratibu za uhamisho wa paundi milioni 34 kuihama klabu yake ya Valencia.Mshambuliaji huyo ambaye pia huchezea timu ya taifa ya Hispania, ameingia mkataba wa miaka minne kuichezea Barcelona na ni usajili wa kwanza msimu huu kufanywa na klabu hiyo, huku Cesc Fabregas ikisemekana pia yupo njiani kujiunga na Barcelona.

Villa, mwenye umri wa miaka 28, anatarajiwa kuwasili Barcelona siku ya Alhamisi kufanyiwa uchunguzi wa afya.

Ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Hispania, alikuwemo katika timu iliyochukua ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 na ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kuwika katika michuano ya Kombe la Dunia.

Kuwasili kwake Barcelona kumezidi kuongeza tetesi za mustakabali wa washambuliaji wawili wa timu hiyo Thierry Henry na Zlatan Ibrahimovic kama wataendela kubakia au la.

Baada ya mkutano wa bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Valencia asubuhi ya Jumatano, Manuel Llorente, Rais wa klabu hiyo inayojulikana pia kwa jina la utani la "Los Che", amesema wamekubaliana na Barca kuwauzia mchezaji huyo.

"Tumemuuza David Villa kwa Barcelona kwa gharama ya euro 40 million," amewaambia waandishi wa habari huko Mestalla.

"Kama kila kila mtu anavyofahamu tungekuwa tumekamilisha mkataba huu tangu mwaka jana, lakini tulidhani wakati ule ilikuwa muhimu kukiweka kikosi chetu kama kilivyo kujaribu kuingia katika ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

"Tumefanikiwa katika lengo hilo na tumemaliza katika nafasi ya tatu katika ligi na Villa amechangia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo hilo. Tunadhani ni biashara nzuri na muhimu kwa hali ya kiuchumi ya klabu."

Rais wa Barcelona anayeondoka madarakani Joan Laporta alidai siku ya Jumanne klabu hiyo "imeridhika" na mchango wa Ibrahimovic wa mabao 21 katika msimu wake wa kwanza tangu alipowasili akitokea Milan.

Henry anaonekana yupo njiani kwenda kucheza ligi ya Marekani maarufu kama Major League Soccer, huku Laporta akifahamisha Wamerekani wakimhitaji Mfaransa.

No comments:

Post a Comment