KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

'Unenguaji si Umalaya, ni kama kazi zingine tu' - Mama Nzawisa

Watu wengi wakituangalia pale jukwaani tunavyonengua kwa umahiri basi wanafikiri kuwa sisi si mali kitu, ndivyo wanavyoanza kusema wanenguaji hao mahiri wa Msondo Ngoma.

Katika mahojiano na Nifahamishe, Mama Nzawisa alisema kuwa yeye muziki ndio kazi yake alianza shughuli ya muziki mwaka 2002 akiwa na bendi ya Mchinga Sound iliyokuwa ikimilikiwa na Mheshimiwa Mudhihiri Mudhihiri ambaye alimpa madaraka Adolf Mbinga enzi hizo wakiwemo akina Muumini Mwinjuma, Roshi Mselera na Maiko Riliko ambao waliifanya Mchinga kuwa juu.

Enzi hizo ukienda pale katika viwanja vya kujidai, Muumini Mwijuma alikuwa akiwapelepaleka wepenzi wa muziki kwa nyimbo zake huku solo lilikuwa likiongozwa na mtu mzima mzee Adalf Mbinga .

Mama Nzawaisa aliendelea kusema "baada ya hapo alijiunga na bendi ya TOT na kuanzia mwaka 2007 nilijiunga na Msondo Ngoma mpaka sasa napatia ugali hapa".

Mama Nzawisa [25] ni mama mwenye watoto watatu na kila mtoto ana baba yake ,mtoto wa kwanza anaitwa Ahmed Hassani,13, wapili Juma Mohamed 11 aliyezaa na mwanandinga wa zamani Mohamed Kimbunga , wa tatu amezaa na mpemba Mohamed Forouk Ally.

Alipoulizwa kwanini kila mtoto ana baba yake alisema kuwa wapenzi wake hao walimkuta akiwa katika fani ya muziki lakini walipofanikiwa kumpata walikuwa wakimkataza asifanye kazi ya muziki jambo ambalo yeye hakukubaliana nalo, "ni hicho tu ndicho kilichonipelekea kuachana na wachumba zangu hao, mwingine alikuwa na wivu kiasi cha kunizushia kuwa natembea na Gurumo na Mabela kutokana uzushi huo nilimwambia kama hanitaki basi aniache niendelee na maisha yangu".

Kweli mimi nimezaa watoto watatu na kila mtoto ana baba yake lakini siyo sababu kwamba wacheza shoo hasa sisi akina dada kuwa ni malaya hapana hiyo ni hulka ya mtu tu mwenyewe sisi hapa wanenguaji wa Msondo tunahakikisha kuwa wapenzi wetu hawatuchoki tukiwa jukwaani na ndiyo maana hata wewe ndugu mwandishi umeona kazi yetu ya kiuno juu kiuno chini kiuno upande kiuno kulia na kushoto hiyo ndiyo kazi inayotuweka mjini kaka, si umalaya.

Kwa upande wa Amina Said au "Queen" mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mama wa mtoto aitwaye Jerome mwenye miaka 5, alisema kuwa kazi ya muziki aliianza siku nyingi baada ya kuhitimu tu shule ya msingi.

Alijiunga na unenguaji katika kundi la msanii Nyamwela ambaye kwa sasa ni mnenguaji wa Bendi ya Twanga pepeta Africa stars.

Amina alisema kuwa baada ya kutoka katika kundi hilo alichukuliwa na bendi ya Bico star mwaka 2002.

Mwaka huo huo nilijiunga na bendi ya Nina Academia, katika bendi hiyo nilikuwa nikifanya vizuri jambo ambalo lilinipelekea kuwa moja ya wacheza shoo tegemeo.

Mwaka 2003 nilichukuliwa na bendi ya Magereza kwa ajili ya kufanya shooting ya video, albamu ilijulikana kwa jina la "Wanawake na Maendeleo", baada ya kumalizika kwa video hiyo nilifuatwa na mwadada mmoja ambaye simkumbuki kwa jina aliyenishauri nijiunge na Msondo.

Nilipofika Msondo nilianza kazi kwa kushirikina na wenzangu lakini cha kushangaza wengi wamekuwa wakiniona kama mtu ambaye ni malaya sana jambo ambalo si la kweli, kwani wacheza shoo siyo malaya ila ukijitakia mwenyewe kwa tamaa zako utakuwa malaya lakini sisi hakuna kitu kama hicho.

"Unaona nimemaliza kucheza naingia kwenye gari la bendi wananirudisha nyumbani" alisema Amina.

Alipoulizwa kuhusu mwanaume aliyezaa naye kama bado wanaendelea na uhusiano au kama ana mpango wa kufunga naye ndoa alisema kuwa mpaka sasa hawapo pamoja kila mtu yuko kivyake.

No comments:

Post a Comment