KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 13, 2010

Tiba za jadi bado zina nafasi muhimu katika zama hizi

Ongezeko la maambukizi ya VVU, gharama kubwa ya tiba kwa wanaougua Ukimwi na idadi ndogo ya madaktari nchini ni baadhi ya sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa wagonjwa wengi kukimbilia kwa waganga wa tiba za jadi ili kupata matibabu.Licha ya wagonjwa wengi kwenda katika kliniki za waganga hao kwa kificho.

Viongozi wa Chama cha Tiba Asilia Tanzania ( ATME) wanafafanua hali hiyo katika makala hii.

Ukiwauliza wagonjwa wengi kwa nini wanajificha wanapokwenda katika kliniki za waganga wa tiba za jadi kupata matibabu, utaambiwa ni kwa sababu wengi wanahusisha uganga na imani za kishirikina au uchawi.

Lakini ukipata nafasi ya kuzungumza na walio bahatika kufika na kupata matibabu katika kliniki hizo, wanakiri tiba za waganga wa jadi ni bora na pengine kuliko hata zinazopatikana katika hospitali za madaktari wa kisayansi.

Wakati mwingine hata kupata dawa za kupunguza makali ya VVU, ARV`s ni vigumu kutokana na kuuzwa kwa bei kubwa kulinganisha na dawa za asili, ambazo matumizi yake hayaambatani na sharti la kula vyakula vya lishe.

Ni kauli ya Mwenyekiti wa ATME, Bw.Simba Abdulrahman, aliyoitoa wakati alipohojiwa ili kujua nafasi ya waganga wa tiba za jadi katika kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa mengine nyemelezi.

``Hapa namaanisha kwamba mgonjwa anayetumia dawa za mitishamba ana nafasi nzuri zaidi ya kuendelea na dawa bila kulazimika kula vyakula maalum vya lishe kwa sababu miti shamba yenyewe ina lishe ingawa si vibaya kwa mgonjwa kutumia vyakula vya lishe,`` alisema.

Akaongeza kuwa, hivi sasa ATME ikishirikiana na wataalam wa tiba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, wapo katika hatua za mwisho kufanikisha tafiti ya dawa za asili zinazoweza kutibu au kupunguza makali ya Ukimwi na magonjwa mengine nyemelezi.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kutambua kuwepo kwa AMTE na katika hatua za awali, jumla ya waganga asilia 52 kutoka AMTE waliingizwa katika mpango huo huku wakihusisha aina ya dawa zaidi ya miti 2000 ya utafiti.

``Baada ya utafiti uliodumu kwa zaidi ya miezi sita, waganga hao walichujwa na kubaki 27 ambapo waliendelea na tafiti hadi kufikia miaka mwili. Mchujo wa mwisho uliwabakisha waganga watano ambapo mmoja wao Bw.Othman Peleu aliwaongoza madaktari kutafiti miti moja kwa moja msituni,`` alisema.

Akaongeza kuwa, utafiti huo uliodumu kwa miaka mitatu ulihusisha dawa zilizopo katika misitu na mbuga za Hifadhi za Taifa ikiwemo ya Vikindu mkoani Pwani na mapori ya mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma ambako dawa kadhaa zilichimbwa na kuvunwa kwa ajili ya utafiti zaidi.

``Kwa sasa utafiti wa dawa hizo umevuka mipaka hadi nje baada ya maabara za hapa nchini kufikia kikomo cha uwezo wake kitaalam,`` alisema.

Bw.Abdulrahman alisema majina ya dawa zote zinazofanyiwa utafiti yapo, lakini kwa sasa AMTE imezuia kuyaweka hadharani kwa kuzingatia haki na sheria za haki miliki hazijawekwa wazi.

Kiongozi huyo , amesema hatua za kuwashirikisha waganga imechukuliwa baada ya kuona idadi kubwa ya wagonjwa wanaokwenda kupata tiba katika kliniki za waganga hao ikiongezeka kila kukicha na wengi wao wanapata mafanikio kiafya.

`` Tanzania ni moja kati ya nchi 46 wanachama wa Chama cha Tiba Asilia Afrika na malengo yamewekwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2015 nchi zote 52 za Afrika ziwe mwanachama wa chama hicho ili kuwa na sauti moja katika harakati za kuboresha tiba asilia,`` alisema.

Wakati hayo yakiendelea hapa nchini, katibu wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Ramadhan Likimangiza alisema mwaka 2002 yalizuka mabishano kati ya waganga wa tiba asilia na madaktari juu ya uwezo walionao wataalam hao asilia katika kutibu maradhi yanayoambatana na Ukimwi kwa mafanikio.

Akasema kutokana na mabishano hayo, ndipo Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, TACAIDS, ilifadhili waganga 52, wawili kutoka kila mkoa kufanya tafiti mbalimbali, zoezi lililotanguliwa na semina ya siku tatu iliyofanyika mjini Kigoma ambapo mkazo uliwekwa kuwezesha waganga kutambua nini maana ya HIV na upungufu wa kinga mwilini.

``Baada ya semina hiyo TACAIDS ilitoa fedha ili kuwezesha Kitivo cha Utafiti na Tiba Muhimbili kuanza tafiti kwa pamoja na ATME ambapo waganga 62 walishirikishwa kikamilifu,`` alisema. Dk.Maneno Tamba, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, kuwepo kwa yote hayo ni dalili njema kuwa tiba asilia inaanza kupata heshima, ingawa bado kuna vikwazo kadhaa hasa kwa baadhi ya viongozi wa halmashauri za wilaya na manispaa waliopewa jukumu la kuwaunganisha waganga wa tiba hizo kupuuza kuwepo kwa waganga hao.

Alisema mwanzoni mwa miaka ya 80 wakati Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere akizindua utafiti wa dawa asilia, aina ya dawa zilizokuwa zikitumika kwa tiba zilikuwa 108, lakini hivi sasa zimeongezeka maradufu hadi kufikia zaidi ya dawa elifu kumi.

`` Vuguvugu la tiba asilia lilianza kuibuka tena mwaka 2002 wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano liliporidhia na kupitisha sheria Na.23 ya Tiba Asilia Mbadala ambapo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alimteua Profesa Rogasia Mahuna kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asilia Tanzania,`` alisema.

Dk.Rama alisema mbali na kuwa mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Mahuna pia yumo katika kundi la wataalam wanaowashauri marais wa nchi 12 za Afrika juu ya matumizi ya Tiba Asilia na pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asilia barani Afrika.

Akasema kwa sasa AMTE ina wanachama zaidi ya 6,000 kote nchini, licha ya kwamba ni mikoa 15 tu Tanzania ndiko kuna matawi na ofisi za mikoa.

SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment