KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, May 19, 2010

Somalia yakerwa na hukumu ya Marekani


Afisa mmoja kutoka Somalia ameikosoa Marekani kwa kumshtaki mtu mmoja kuhusika na uharamia katika pembe ya Afrika.


Abdiwali Abdiqadir Muse
Jamaal Cumar, afisa wa Kisomali aliyopo Marekani, ameiambia BBC kulikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya mamlaka ya kisheria katika kesi ya Abdiwali Abdiqadir Muse.

Bw Cumar amehoji mamlaka yeyote ya kigeni kuwashtaki maharamia wa Kisomali nje ya pwani ya Afrika Mashariki.

Amesema anataka mahakama ya kimataifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kushughulikia kesi za maharamia.

Washukiwa wa uharamia wa Kisomali wameshtakiwa nchi mbali mbali dunaini, kutokana na Somalia kutokuwa na serikali thabiti.

Wataalamu wa kisheria wamekuwa wakipata tabu kujua wapi wawashtaki maharamia kwa miaka mingi.

Majeshi ya kigeni yamekuwa yakiwakamata maharamia mara kwa mara katika pwani ya Somalia, yakiwanyang'anya silaha zao na kuwarejesha baharini kutokana na kukosekana mamlaka maalum ya kuwashughulikia.

Jaribio la hivi karibuni la kuunda mahakama ya kimataifa imeshindikana kwasababu ya kukosa fedha.

'Samahani sana'
Muse amekiri makosa yake katika mahakama ya New York kwa kukamata meli ya Marekani na kumteka kapteni wake mwaka jana.

Abdiwali Abdiqadir Muse sasa anakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka 27 gerezani. Anatarajiwa kuhukumiwa mwezi Oktoba.

Muse ni mshambuliaji pekee aliye hai baada ya kutokea tukio hilo katika meli ya mizigo ya Maersk Alabama kwenye pwani ya Somalia mwezi Aprili 2009.

Alikamatwa na askari wa majini wa Marekani, ambapo walenga shabaha wao waliwaua maharamia wengine watatu waliokuwa wakijaribu kutoroka kutumia boti okozi ili kumwokoa kapteni.

Wakati wa kusikilizwa kesi kwenye mahakama ya Manhattan,waendesha mashitaka wamemwelezea Muse kama kiongozi wa maharamia wenzake wanne walioiteka meli ya Maersk Alabama kilomita 450 kutoka pwani ya Somalia.

Pia wamesema kuwa Muse alikuwa wa kwanza kupanda meli hiyo, huku akimfyatulia risasi kapteni Richard Phillips kwa kutumia bunduki aina ya AK-47.

Siku ya Jumanne, Muse alisema kupitia mkalimani : "Ninaomba radhi sana kwa mambo tuliyoyafanya. Yote haya yametokana na matatizo tulionayo Somalia."


Inasemekana kuwa ni kesi ya kwanza ya uharamia kusikilizwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita Marekani.

Meli hiyo, iliyokuwa imebeba chakula cha msaada, ilitekwa na maharamia hao wanne Aprili 2009.

Kapteni Phillips aliwaambia mabaharia wake wajifungie kwenye chumba kisha yeye akajisalimisha kuwalinda watu wake.

Alichukuliwa mateka katika boti okozi ambapo baadae walizingirwa na meli za kivita za Marekani na helikopta.

Purukushani hiyo iliisha siku chache baadae wakati walenga shabaha wa jeshi la majini walipowaua maharamia watatu, na kumwokoa kapteni.

No comments:

Post a Comment