KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 20, 2010

Sakata la Kuulipua Ubalozi wa Marekani Wanafunzi 8 Wakamatwa, Ubalozi Watoa Taarifa

WANAFUNZI wengine wapatao wanane wa shule ya Sekondari Biafra wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano maalum kuhusiana na jaribio la kulipua ubalozi wa Marekani.
Wanafunzi hao walikamatwa jana majira ya alasiri wote wakiwa wanafunzi wa shule hiyo na wanahojiwa chini ya maofisa wa usalama wa taifa wakishirikiana na polisi.

Awali Jumapili majira ya saa 3 usiku, mwanafunzi wa kidato cha pili, Nassib Zukheri [16] wa shule hiyo alikamatwa katika ubalozi huo akiwa katika jaribio la kuuteketeza ubalozi huo kwa mabomu ya mafuta ya taa.

Taarifa za awali zilisema kuwa mwanafunzi aliyekamatwa alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Mtambani lakini taarifa za polisi zimethibitisha kuwa mwanafunzi huyo ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Biafra.

Pia taarifa za awali zilisema kuwa mwanafunzi huyo aliingia ubalozini wakati walinzi wakiwa wamelala lakini ubalozi wa Marekani umekanusha mwanafunzi huyo kufanikiwa kuingia ndani ya ubalozi na leo umetoa taarifa ifuatayo kwa vyombo vya habari.

TAARIFA YA UBALOZI WA MAREKANI DAR

-----------------

Siku ya Jumapili, tarehe 16 Mei, mnamo saa 2.30 usiku, mvulana mwenye umri wa miaka 15 alikimbia na kumpita mlinzi aliyekuwa mbele ya Ubalozi wa Marekani, akawasha moto kwenye chupa iliyokuwa na mafuta ya taa na kisha kuirusha chini ya moja ya malori mawili ya kubebea maji yaliyokuwa yameegeshwa nje ya ukuta wa Ubalozi.

Chupa hiyo ilivunjika lakini haikuweza kulipua moto. Walinzi wa Kampuni ya KK wanaolinda ubalozini hapo walimkamata mara moja kijana huyo kabla hajaweza kurusha chupa ya pili.

Hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa wala mali yoyote iliyoharibiwa katika tukio hilo. Askari wa Jeshi la Polisi la Tanzania aliwasili sehemu ya tukio sekunde chache baadaye na kumkamata mtuhumiwa. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.

Baadhi ya maelezo yanayotolewa kuhusu tukio hili si sahihi, yamekuzwa na kutiwa chumvi mno na yasiyo ya kweli, yakidai kuwa mvulana huyo aliingia ndani ya ubalozi. Hii si kweli. Hakukuwa na mtu yeyote aliyeweza kuingia ndani ya Ubalozi wa Marekani.

Taratibu zetu za kiusalama za kuzuia wahalifu kuingia ubalozini zilidhihirisha ufanisi wake hapo Mei 16.

Walinzi wa kampuni ya KK na Polisi wa Tanzania walishughulikia suala hili kwa weledi mkubwa. Tunawashukuru sana.

No comments:

Post a Comment