KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 15, 2010

Rais Jakaya Kikwete, akiwaaga viongozi wa madhehebu ya dini


Apanga kukutana nao mara mbili kila mwaka
Asema alitumiwa sms nyingi za malalamiko
Waziri Philip Marmo azongwa, atoboa siri


Rais Jakaya Kikwete, akiwaaga viongozi wa madhehebu ya dini baada ya kupokea maazimio yaliyotolewa na viongozi hao wakati wa semina iliyomalizika jana.
Rais Jakaya Kikwete ameahidi kushirikiana na viongozi wa dini kama wadau muhimu wa kuhubiri amani, upendo, umoja na maendeleo, majukumu ambayo hata serikali pia inayahimiza.

Ili kuimarisha ushirikiano huo, Rais Kikwete amesema Serikali itaweka utaratibu wa kukutana nao mara mbili kila mwaka na kuwashirikisha katika masuala yote muhimu ya kitaifa.

Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam jana, baada ya kupokea maazimio ya semina ya siku mbili kwa viongozi wa dini ambayo iliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Viongozi wa dini wameitaka serikali kuweka utaratibu wa kukutana nao, kutumia mtandao wao kwa kupanua wigo wa ushiriki, kuwashirikisha katika masuala ya kitaifa kuanzia hatua za awali pia wameahidi kutoshabikia siasa katika nyumba za ibada.

Maazimio hayo ambayo yalisomwa na Askofu Dk. Owedemburg Mdegella, yaliwakataza viongozi wa dini kushabikia siasa katika nyumba za ibada, taasisi za kidini kushirikiana kuandaa mikakati ya kurejesha maadili ya taifa na kuitaka serikali kuyatekeleza.

Alisema Serikali inathamini sana mchango wa mashirika ya dini katika nyanja za kijamii ikiwemo sekta za elimu na afya na hasa kuchochea maendeleo ya taifa. Alisema uhusiano kati ya serikali na viongozi hao kamwe hauwezi kuvunjwa na tofauti mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea kutokana na maamuzi yanayofanywa na Serikali.

"Tunajua wakati mwingine tumekuwa tukitofautiana kutokana na maamuzi yetu (Serikali) kama wakati TRA ilipotaka kuwatoza kodi, lakini tulikaa tukazungumza na kuafikiana...jambo muhimu hapa tusiache tofauti zetu kuwa chanzo cha chuki na mtafaruku," alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa milango iko wazi kwa viongozi wa dini kupata ufafanuzi wa jambo lolote serikalini hasa wanapoona serikali ikifanya maamuzi ambayo hayawapendezi.

"Nimefurahi sana kwa kuwa huu ni mkutano wa kwanza kwa mimi kukutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja, nawaomba tushirikiane na mkiona serikali inafanya jambo haliwapendezi, serikali ni ya watu ambao ni waumini wenu, watumeni na ujumbe utanifikia tu...lakini simu yangu ipo wazi wakati wote mnaweza kunitumia ujumbe mfupi na mimi nitajibu," alisema.

Akizungumzia utaratibu wa kukutana na viongozi wa dini mara mbili kila mwaka, alipendekeza kuonana na kila madhehebu kwa wakati wao na mkutano wa pili ukutanishe wote kwa pamoja.

"Nasema hivi kwa sababu nimepata meseji nyingi sana kutoka kwa Waislam na Wakristo ambao hawakuhudhuria hapa, wengi wamelalamika wakisema 'kila mara nyinyi na Bakwata tu mnatudharau' na wengine wakisema 'hata sisi ni maaskofu'...mimi nimewatoa hofu kwa kuwaambia tu kwamba tutawapa nafasi ya kukutana nao kwa kuwa huu ni mwanzo," alisema.

Kuhusu viongozi wa dini kushabikia siasa, alisema serikali inaheshimu uhuru wa kuabudu, lakini haitavumilia kejeli na kashfa dhidi ya dini nyingine na kwamba itawachukulia hatua wale watakaofanya hivyo.

Akizungumzia mmomonyoko wa maadili, alisema tatizo hilo ni kubwa na kuomba ushirikiano wa viongozi hao ili kuyarejesha.

"Jamii yetu inapita kwenye matatizo makubwa sana, hili la kuyarejesha naliafiki. Tuhakikishe kwamba mnawaeleza waumini wenu suala hili ili wakipewa kazi wasidokoe wala wasile rushwa," alisema.

Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, alisema serikali imejipanga kuhakikisha kwamba wananchi wote wenye sifa ya kupigakura wanapata fursa hiyo.

Alisema serikali inaendelea kufanya marekebisho kwenye sheria ya uchaguzi ili kuweka uwanja sawa kwa wagombea na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye uchaguzi.

Hata hivyo, alisema pamoja na kwamba sheria imefuta takrima, lakini kuiondoa imekuwa tabu kutokana na mila na desturi za makabila kadhaa. "Kuna mazingira maalum kama Kilimanjaro huwezi kuita wazee bila mbege na kwao hiyo ni kawaida hawaioni kama ni rushwa," alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao kuchagua viongozi waadilifu na kuwataka wagombea kukubali matokeo baada ya uchaguzi. Akitoa neno la shukurani, Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi, Dk. Gerald Mpango, alimshukuru Rais Kikwete kwa kuthamini mchango wao na kufungua milango kwa ajili ya kuwasikiliza.

Alisema Rais Kikwete ni kiongozi wa pekee anayefaa kuigwa kwa kuwa mwananchi yeyote anaweza kuwasiliana naye na akamsikiliza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajab Kiravu, amesema kuwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu, utagharimu Sh bilioni 78 ikilinganishwa na Sh bilioni 62.5 zilizotumika mwaka 2005.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema mbali ya vyama 18 ambavyo vimesajiliwa, kuna maombi mengine mapya saba ya vyama vinavyoomba usajili.

Katika tukio lingine, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini wamemvamia Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, na kutishia kususia kuandika habari za ofisi ya Waziri Mkuu baada ya waziri huyo kuwazuia kuingia kwenye mkutano wa viongozi wa dini na serikali.

Waandishi hao ambao juzi walifukuzwa kwenye mkutano huo, jana walifika kwenye mkutano huo mapema na kumsubiri Waziri Marmo ili kupata ufafanuzi wa sababu za wao kuzuiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo. Baada ya waziri huyo kuwasili, waandishi walifunga njia na kumhoji lakini alitaka kuacha kuwajibu kwa maelezo kwamba anahitajika kwenye mkutano jambo ambalo liliwakera waandishi na kumzuia.

Baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa takribani dakika tano hivi, Waziri Marmo aliwaruhusu kuingia kwenye mkutano huo na baada ya mkutano aliwafuata na kuwaeleza kwamba alilazimika kuwatoa nje baada ya hali ya hewa ndani ya mkutano kuchafuka.

"Kama mwenyekiti wa mkutano nisingeweza kuwaruhusu kukaa wakati hali ya hewa imechafuka, niliona hakuna faida ya ninyi kusikiliza mambo yale na kuyatangaza kwa sababu yangetoa picha mbaya sana," alisema.


SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment