KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, May 19, 2010

Njama ya al-Qaeda Kombe la Dunia yatibuka

Anayedaiwa kuwa mfuasi wa al-Qaeda aliyetiwa kizuizini Iraq ametoa maelezo juu ya mpango wa kutaka kufanya shambulio Kombe la Dunia Afrika Kusini mwezi ujao.

Mtu huyo raia wa Saudi Arabia, Abdullah Azam Saleh al-Qahtani, amewaambia waandishi wa habari alipanga kushambulia timu ya Uholanzi na Denmark kwa kulipiza kisasi baada ya kuchora vibonzo vya mtume Muhammad.

Lakini amesema viongozi waandamizi wa al-Qaeda bado hawakuidhinisha mpango huo.

Siku ya Jumatatu polisi wa Iraq walidai wamezuia shambulio kufanyika Kombe la Dunia.

Madai hayo yaliibua simu kutoka polisi wa Afrika Kusini, kuTAKAujua kinachoendelea.

'Mashabiki waliolengwa'
Bw Qahtani alikamatwa baada ya majeshi ya Iraq kuona karatasi iliyoelezea mpango mzima uliofanywa mafichoni kunakotumiwa na viongozi waandamizi wawili wa al-Qaeda, waliouawa Aprili.

Bw Qahtani ameliambia shirika la habari la AP, " Tulizungumzia swala la kulipiza kisasi kutokana na kumdhalilisha mtume kwa kuishambulia Denmark na Uholanzi."

"Kama tusingeweza kufikia timu zao, basi tungewalenga mashabiki."

Mpango huo ungehusisha mabomu ya magari na mashambulio kwa kutumia bunduki.

Bw Qahtani amesema mpango haukuidhinishwa, lakini alikuwa anasubiri idhini kutoka kwa kiongozi wa pili wa al-Qaeda, Ayman al-Zawahiri.

Maelezo kufichuliwa
Haina uhakika iwapo al-Qaeda ya Iraq ina raslimali za kufanya shambulio kama hilo kwenye eneo lililo mbali na kituo chao.

Nyaraka iliyokuwa na maelezo ya mpango huo na jina la Bw Qahtani, ilipatikana kwenye harakati za pamoja za Marekani na Iraq ambapo kiongozi wa al-Qaeda Abu Ayyub al-Masri na Abu Omar al-Baghdadi waliuawa.

Bw Qahtani alikamatwa na mamlaka ya Iraq Mei 3.

Mwaka 2006 gazeti la Denmark lilichapisha vibonzo 12 ikimwonyesha Mtume Muhammad, ikiwemo moja inayomwonyesha akiwa na bomu kwenye kilemba chake.

Huko Uholanzi, wanasiasa wanaopinga Uislamu wamekiita kitabu takatifu cha Quran "kitabu cha kifashisti."

Fifa imesema haitAtoa maelezo yeyote kuhusu vitisho vyovyote dhidi ya Kombe la Dunia.

Msemaji wa polisi wa Afrika Kusini Vish Naidoo amesema polisi wa nchi hiyo walisikia kuhusu mpango huo kupitia vyombo vya habari na hawakupata taarifa zozote kutoka serikali ya Iraq.

Bw Qahtani aliwasili Iraq kutoka Saudi Arabia mwaka 2004 baada ya uvamizi wa Marekani. Alikamatwa mwaka 2007 na kushikiliwa kwenye kambi ya Bucca kwa miaka miwili.

No comments:

Post a Comment