KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 3, 2010

Mapacha walioungana waeneza Uislam


Mapacha walioungana kutoka Cameroon Pheinbom na Shevoboh walionekana kama nuksi walipozaliwa, lakini mafanikio yao ya kutenganishwa na madaktari wa Saudi Arabia yamebadili kabisa maisha yao – na imani ya baadhi ya watu katika kijiji chao.

Walipozaliwa walikuwa wameungana kwenye kifua, tumbo na nyonga na baadhi ya wauguzi katika kijiji cha Babanki Tungo kilichopo kaskazini-magharibi mwa Cameroon, walishtushwa sana na hivyo kukimbia siku walipozaliwa.
Huduma muhimu za matibabu huko Babanki Tungo hazikuwa na ufanisi kwa mabinti hao, kufuatia ombi kupitia mtandao, mfalme wa Saudi Arabia alikubali kuwalipia nauli ili waende nchini humo kwa ajili ya upasuaji mwaka 2007.

Upasuaji huo uliochukua saa 16 ulifanikiwa kuwatenganisha mapacha hao na kwa sasa kila mmoja ana tumbo lake.

Hata hivyo, miaka mitatu tangu upasuaji huo ufanyike, changamoto nyingi bado zinawakumba.

Baada ya upasuaji huo, kila binti alibaki na mguu mmoja tu, na kwa sasa wanasubiri kurudi Saudi Arabia ili wabandikwe viungo bandia na waanze kujifunza kutembea.

Kwa sasa wanaweza kutambaa tu. Pamoja na hayo mabinti hao wanapenda kucheza, ni wachangamfu, na watundu, kama ambavyo ingetarajiwa kwa mtoto yeyote mwenye umri wa miaka minne.
Kubadili kuwa muislamu

Baadhi ya watu huko Babanki Tungo- kijiji kinachojishughulisha na kilimo na hasa uzalishaji wa mboga za majani walidhani kuwa watoto hao ni ‘zawadi kutoka kwa shetani’ ambao wameletwa kumwadhibu baba yao, ambaye tayari ana watoto wengine 13 kutoka kwa wake zake wawili.

Wengine waliamini kwamba Pheinbom na Shevoboh wamezaliwa kuadhibu kijiji kizima, baada ya kiongozi mmoja wa kimila eneo hilo alipochomwa moto akiwa hai na watu wenye hasira.

Mama wa mabinti hao Emerencia Nyumale anakumbuka kwa kusema “Ulikuwa wakati mgumu wakati watoto hawa bado walikuwa wameungana.”

Anasema, “Watu walikuwa wakiniona nikiwabeba na kukimbia na nilikuwa nikijihisi nimekosa na mpweke.”
Nashukuru Mungu hayo yote yamekwisha tangu watenganishwe.”

Mkasa wa watoto hawa umeleta jambo jengine muhimu kwa watu wa Babanki Tungo.

Serikali ya Saudi Arabia inafadhili kituo cha kiislamu katika kijiji hicho chenye msikiti, shule ya chekechea na msingi na pia kituo cha afya.
Hatua hii imesababisha baadhi ya wazee kutabiri kuwa wengi waliopo Babanki Tungo kwenye imani nzito ya kikristo kutabadilka kuenea kwa uislamu.

Kama njia ya kushukuru fadhila ya mfalme huyo, familia hiyo imebadilisha dini na kuwa waislamu.

Baba wa watoto hao, Ngong James Akumbu, sasa anajiita “Abdallah”, Emerencia naye ni “Aisha”, na watoto wao watano wanakwenda kwenye shule ya msingi ya kiislamu.

Baraka au laana?
Kum Edwin, ambaye ni mwalimu katika shule hiyo, naye pia amebadili dini na kuwa muislamu.

Bw Edwin, aliyebadili jina lake na kuwa “Abdallah Waqf” amesema, “Kabla ya shule hiyo kuanzishwa, nilikuwa sina ajira, nilikuwa na wapenzi wengi na nilikuwa nakunywa sana pombe.”

“Niliposikia kunaanzishwa shule ya kiislamu, nilichukua mafunzo ya kiislamu kwa miezi mitatu, siku hizi sinywi sana na kwa sasa natafuta mke kwa sababu kuwa na wapenzi wengi sio vizuri.”

Watu wengi Babanki Tungo wanaona kuzaliwa kwa Pheinbom na Shevoboh ni kama baraka badala ya laana.

Macho ya wasiwasi waliokuwa wakitazamwa mapacha hao na wanakijiji imeacha.

Baba wa watoto hao alisema, “Huwa namwambia kila mzazi awe na subra kwasababu Mungu mara nyingi humletea mwanadamu mambo mazito ambayo baadae hugundua kuna kheri.”

Hakika, mapacha hao wameona mabadiliko makubwa katika maisha yao.

Kwa kutengwa walipozaliwa, sasa wana maisha yao pekee na wamechangia kwa kiasi kikubwa kubadili maisha ya watu wanaowazunguka.

Baada ya yote hayo waliyoyapitia, kujifunza kutembea kunaweza kuwa rahisi kwao.

No comments:

Post a Comment