KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 11, 2010

Malawi Nchi Yenye Wanawake Wengi Kupiga Marufuku Ndoa za Wake Wengi


Malawi nchi ambayo ina idadi kubwa sana ya wanawake kuliko wanaume, inatarajia kupitisha sheria itakayowapiga marufuku wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja hali ambayo imeamsha hasira za wanaume wa kiislamu nchini humo.
Serikali ya Malawi inatarajia kupiga marufuku wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja hali ambayo imewakasirisha waislamu ambao idadi yao ni ndogo sana nchini Malawi.

Msemaji wa Umoja wa Waislamu nchini Malawi akiongea na shirika la habari la BBC la Uingereza alisema kwamba sheria hiyo itakapopitishwa itakuwa ikiwabagua waislamu wa nchini humo.

Msemaji huyo alisema kwamba Malawi ina wanawake asilimia 6 zaidi ya idadi ya wanaume hivyo kama wanaume watazuiliwa kuoa mke zaidi ya mmoja basi wanawake wengi watabaki bila kuolewa na matokeo yake kugeuka makahaba.

Akiongelea sheria hiyo mpya, waziri wa masuala ya jamii wa Malawi, Patricia Kaliati, alisema kwamba serikali ya Malawi imepanga kupiga marufuku wanaume kuoa zaidi ya mke mmoja ili kuwalinda wanawake na manyanyaso wanayoyapata katika ndoa za mitala.

Waziri huyo alisema kuwa tatizo hutokea kwakuwa wanaume hawawezi kuwapenda na kutoa mapenzi yao sawa kwa mwanamke zaidi ya mmoja.

"Wakati mwanaume anapokuwa na wake wawili, watatu au wanne huwa hamna ushirikiano, mwanamke mmoja hupendelewa zaidi kuliko wenzake", alisema waziri Patricia.

Hata hivyo katibu wa umoja wa Waislamu nchini humo, Imran Shareef Muhammed aliipinga sheria hiyo akisema kuwa mbali ya waislamu kuna makabila mengi yanayoruhusu ndoa za mitala ambayo nayo yanaipinga sheria hiyo.

"Kama watapiga marufuku ndoa za mitala itamaanisha kuwa wanawake wengi watageuka machangudoa", alisema katibu huyo wa waislamu.

"Kila mwanamke ana haki ya kuolewa na kuwa chini ya hifadhi ya mumewe".

"Kwa mujibu wa sheria za kiislamu ndoa za mitala si lazima hivyo mwanaume halazimishwi kuoa mke zaidi ya mmoja, ingawa mwanaume anaruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja iwapo ana uhakika ataweza kuwapa haki sawa wake zake", aliendelea kusema katibu huyo wa waislamu.

Iwapo sheria hiyo mpya itapitishwa, wanaume ambao tayari wapo kwenye ndoa za mitala sheria hiyo haitawagusa lakini wale watakaotaka kuongeza mke baada ya sheria hiyo kupitishwa huenda wakatupwa jela.

No comments:

Post a Comment