KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 15, 2010

Leo jioni, michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati


Leo jioni, michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame, inaanza kutimua vumbi kwenye viwanja vya Amahoro na Nyamirambo vilivyopo katika jiji la Kigali nchini Rwanda.

Katika ufunguzi wa michuano hiyo leo, wenyeji APR watacheza dhidi ya Vital’O’ kutoka Burundi huku Simba walio katika Kundi C la michuano hiyo, wakitarajiwa kushuka dimbani Jumatatu na kucheza dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, klabu ya Atraco ya Rwanda.

Aidha, wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, klabu ya Mafunzo kutoka Zanzibar, watashuka dimbani kesho kucheza mechi yao ya kwanza katika Kundi B kwa kuvaana na Heartland kutoka Nigeria, ambao walialikwa ili kuongeza msisimko katika michuano hiyo, kama ilivyo kwa mabingwa wa msimu uliopita wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, klabu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Sisi tunawatakia mema ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba pamoja na Mafunzo, kwani wao ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano hiyo.

Zaidi, sisi tunaungana na Watanzania wengine kuwaombea kheri Simba na Mafunzo kwa kutambua kwamba michuano hiyo ndiyo pekee itakayokuwa na nafasi ya kupunguza machungu ya kutolewa katika mashindano mengine yote ya kimataifa.

Tunakumbuka kwamba Yanga na Mafunzo waliokuwa wakituwakilisha katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, walitolewa kwa vipigo vya 4-2 na 6-1 kutoka kwa FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na The Gunners ya Zimbabwe.

Hatujasahau vilevile kwamba ni juzi tu, Simba na klabu ya Miembeni ya Zanzibar, walitolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa vipigo vibaya vya magoli 6-3 na 6-2 kutoka kwa waliokuwa wapinzani wao, timu za Haras El Hodoud na Petrojet, zote kutoka nchini Misri.

Ni kwa sababu hiyo ya kutokuwa na matumaini yoyote katika michuano ya kimataifa baada ya timu zote kutolewa, ndipo tunapojawa na hisia kali za kutaka kuziona klabu za Simba na Mafunzo zikifanya vyema katika Kombe la Kagame.

Tunaamini kwamba wachezaji wa timu hizo wakijituma na kutumia vyema vipaji vyao uwanjani, watapata ushindi katika kila mechi na kutupa ahueni juu ya ‘msiba’ wa kutolewa kirahisi katika michuano mikubwa ya Klabu Bingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho.

Hakuna kinachoshindikana. Simba, ambao kihistoria ndio wanaoongoza kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa michuano hiyo baada ya kubeba kombe mara sita, watakuwa na fursa ya kurejea mafanikio yao ya nyuma kwa kuongoza Kundi C na kusonga mbele hadi fainali.

Kwa dua zetu, tunaamini kwamba Mafunzo pia wataongoza Kundi B, kufuzu hatua za robo fainali na nusu fainali kabla kukutana na ‘ndugu’ zao Simba katika fainali.

Kwa mazingira kama hayo, ya timu mbili za Tanzania kuingia fainali, sisi na Watanzania wengine tutajawa na furaha kubwa kwani uhakika wa kuuleta nchini ubingwa wa michuano hiyo utakuwa ni wa asilimia zote.

Hata hivyo, wakati sisi tukitazamia mafanikio makubwa ya klabu za Simba na Mafunzo katika michuano hiyo inayodhaminiwa na Serikali ya Rwanda kwa ushirikiano na rais wao Paul Kagame, ni jukumu la wachezaji wa timu zote mbili kuhakikisha kwamba hawatuangushi.

Tunapenda kuwakumbusha kwamba mpira ni magoli. Hivyo, ni wajibu wa washambuliaji na kila mchezaji kuhakikisha kwamba anatumia nafasi zote zitakazojitokeza. Mbali na kutumia vyema nafasi watakazopata ili kufunga magoli mengi kadri itavyowezekana, mabeki wa Simba na Mafunzo watapaswa pia kuwa makini na kuepuka uzembe wowote utakaowazawadia wapinzani wao magoli ya kirahisi.

Chondechonde. Wachezaji wa Simba na Mafunzo fanyeni kila mnaloweza kuhakikisha kwamba mnacheza soka safi na kutupa raha Watanzania.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu zibariki Simba na Mafunzo.

No comments:

Post a Comment