KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Wednesday, May 19, 2010

Jonathan aungwa mkono na wapiganaji


Aliyekuwa mpiganaji wa Niger Delta amesema Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ni mtu anayefaa kusuluhisha mgogoro wa eneo hilo linalozalisha mafuta mengi.

Victor Ebokawe, ambaye pia anajulikana kama Jenerali Boyloaf, ameiambia BBC, kwasababu Rais Jonathan anatoka eneo hilo, basi ana uelewa zaidi kuhusu matatizo yake.

Bw Ebokawe amesema Bw Jonathan anatakiwa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Wapiganaji wamefanya mashambulio mara kadhaa yaliyosababisha Nigeria kupoteza mamilioni kutokana na mapato ya mafuta yaliyopotezwa katika kipindi cha miaka mingi iliyopita.

Hakuna kitakachomzuia.Hawezi kutuambia kuwa hatogombea.
Victor Ebokawe
Mwaka jana, maelfu ya wapiganaji walisalimisha silaha zao kwa ahadi ya kupewa mafunzo na ajira badala yake.

Lakini mpango huo ulianza kuonyesha dalili za kutikisika wakati wa ombwe iliyokuwepo baada ya aliyekuwa Rais Umaru Yar'Adua kuanza kuugua.

Alifariki dunia mapema mwezi huu na Bw Jonathan aliapishwa kuwa Rais badala yake.

Siku ya Ijumaa, Rais Jonathan alitemebela Niger Delta na kutaka mpango mzima wa kutoa msamaha uimarishwe.

Bw Ebokawe, kiongozi wa Movement for the Emancipation of the Niger Delta, aliyesema amezungumza na Bw Jonathan, anaamini viongozi wa Niger Delta watashirikiana na Rais huyo wakati akijaribu kutekeleza mpango huo wa kutoa msamaha.

Bw Jonathan hajasema iwapo atagombea kiti cha urais mwakani na chama tawala cha People's Democratic Party (PDP) kimesema mgombea wake atatokea kaskazini, na si kusini kama yeye.

Bw Ebokawe ameiambia BBC, " Hakuna kitakachomzuia.Hawezi kutuambia kuwa hatogombea."

" Bw Jonathan ni mtu ambaye yuko tayari kuiongoza Nigeria kama Nigeria moja."

Wapiganaji hao wanasema wanafanya kampeni ili utajiri wa mafuta wa Nigeria utumike zaidi kuwanufaisha raia wa huko lakini wachambuzi wanasema mashambulio na vitendo vya utekaji nyara vinafanywa na wahalifu wanaodai kulipwa kikombozi.

No comments:

Post a Comment