KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, May 22, 2010

Heshima na Uvumilivu Umenifanya Nifike Mbali -Msanii Elias Barnabas

Kijana machachari katika fani ya muziki wa kisasa kwa hapa bongo tunauita muziki wa kizazi kipya, Elias Barnaba aka Barnabas aliyetamba sana na nyimbo yake 'Njia Panda' amesema kwamba heshima na uvulimu alionao ndio chanzo cha mafanikio yake kiasi cha kualikwa na mwanamuziki maarufu wa Kongo Fally Ipupa kurekodi nyimbo pamoja.

Barnabas alizaliwa miaka 19 iliyopita katika jiji la Dar es Salaam ,wazazi wake wakiwa wenyeji wa mkoa wa Morogoro kabila la wapogoro.

Elias akiwa mtoto wa kwanza katika familia yao alipata bahati ya kumaliza elimu ya msingi na baada ya hapo alijiunga na sekondari ya Mikoji ambapo aliacha shule alipokuwa kidato cha pili na kuamua kujikita katika fani ya muziki.

Uamuzi wake huo ulipingwa vikali na wazazi wake ambao walitegemea angejikita zaidi kwenye elimu kwa kuwa waliamini elimu ndio msingi wa maisha.

Katika kipindi chote hicho Barnabas alijikita zaidi kwenye muziki kwa kuwa ndio ulikuwa hobi yake ingawa alikuwa hajui apitie wapi ili afike kileleni.

Mambo yakienda tofauti na alivyotegemea Barnabas aliamua kufanya maonyesho mbalimbali katika kumbi tofauti za hapa bongo Dar es Salaam.

Mungu si Athumani mwaka 2007 alifanikiwa kusaini makataba katika Shule ya kukuza vipaji vya muziki hapa nchini Tanzania House of Talent (THT) shule hiyo ipo chini ya Mkurugenzi Ruge Mutahabwa.

Barnabas alisema kwamba jukumu la kwanza la THT lilikuwa ni kumsaidia kimawazo na kumpa elimu ya muziki ambayo hivi sasa anamini kabisa ndio chanzo cha mafanikio yake.

Elias Barnabas tayari ameshatunga nyimbo zaidi ya kumi kiasi cha kumfanya awe na albamu ambayo mpaka sasa hajaipa jina wala kufanya uzinduzi, lakini tayari nyimbo zilizomo katika albamu hiyo zimeshaanza kukonga nyoyo za watanzania.

Barnabas anatamba hivi sasa na nyimbo yake ya NJIAPANDA akiwa amemshirikisha mwanadada Dorine Kasia Pipi.

Nyimbo nyingine za Barnabas ni Kodi mangasubi, mbalimwezi, nivumilie, nimelimiss, beby i love, mdomo, mwongo, dukuduku na huruma.

Wimbo wa Njiapanda umekubalika sana kiasi cha kumfanya ashindwe hata kupata siku ya mapumziko kutokana na mialiko mingi katika matamasha.

Barnabas anasema kuwa hali hii imemfanya ajitume ili aweze kuwa kama wengine ambao kwa sasa wana mafanikio makubwa ya kimuziki.

Kutokana na kipaji alicho nacho Barnabas na gwiji la muziki wa dansi toka nchini Kongo Fally Ipupa alimwagia sifa kibao Barnabas na kumwahidi atarekodi naye nyimbo na kumtumia mialiko ya kwenda nchini Kongo.

Ipupa alikutana na Barbas wakati alipokuja Tanzania kufanya shoo pamoja na Mbilia Bel mwaka jana.

No comments:

Post a Comment