KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 22, 2010

Emanuel Okwi - Mshambuliaji Mwenye Kasi Anayewatia Wazimu Simba

TANGU alipokuwa katika timu yake ya zamani SC Villa ya Uganda, Emmanuel Okwi, mchezaji ambaye kwa sasa ana mchango mkubwa katika kikosi cha timu ya Simba, alikuwa mwiba mchungu kwa maadui.

Mara zote alifahamika kwa staili yake ya kucheza kwa kasi, akimiliki mpira kwa namna iliyomfanya awe na namba ya kudumu katika kikosi cha timu hiyo na pia akifunga mabao mazuri yaliyoifaidisha timu yake hiyo.

Kwa umahiri wake, akajikuta akiitwa mfululizo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes,' sambamba na wakali wengine kama akina Dan Wagaluka, Steven Bengo na wengineo.

Na alipotua Simba mwanzoni mwa msimu huu, Okwi akaendeleza mambo yake.

Hadi sasa amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao uwezi wao unakubalika kwa asilimia 100% na kocha Mzambia Patrick Phiri na pia mashabiki wa timu hiyo.

Staili yake ya kukimbia na mipira kutoka kushoto hadi kulia mwa uwanja, kutoa vyumba safi na mashuti yake ya kustukiza vimeendelea kumuweka katika kundi la wachezaji 'nyota' wa timu hiyo.

Phiri pamoja na mashabiki wote wa Simba wamekuwa wakivutiwa na vitu vyake 'adimu,' hasa kasi yake na uwezo wa kumiliki mpira ambao huleta kashakash za mabao langoni mwa maadui.

Katika moja ya vitu vyake adimu, Okwi ndiye aliyesababisha Simba ikapata penati ambayo ilizaa bao la kufutia machozi siku ilipolala 2-1 dhidi ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Tusker.

Itakumbukwa pia kwamba Okwi alitoa pia mchango mkubwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, kilichofanikiwa kutwaa taji la ubingwa wa michuano ya Chalenji, iliyomalizika hivi karibuni nchini Kenya.

Katika mojawapo ya michango yake, Okwi akiwa ameingia kipindi cha pili, aliweza kuipatia timu hiyo bao la pili la ushindi baada ya kuwalamba chenga mabeki wote wa Rwanda kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Na katika safari ya Simba hiyo ya kuelekea kwenye taji la ubingwa Okwi amekuwa kiungo muhimu katika nafasi ya ushambuliaji ambapo huchangia katika kuleta ushindi.

Hana namba maalumu kwani pindi mpira unapoanza, utamwona mara yuko upande wa kushoto kama winga mshambuliaji, au katikati akicheza namba 9 na 10 na wakati mwingine kama winga wa kulia ili mradi tu anahaha kuisumbua ngome ya timu pinzani.

Kuhusu jezi, alipotua Simba alikuwa akivaa jezi namba 29, lakini katika michuano ya Kombe la Tusker, alikuwa akivaa jezi namba saba.

Mwenyewe anasema amependelea kuvaa jezi hiyo namba saba kwa vile ni mfuasi mzuri wa winga wa zamani wa Manchester United Cristiano Ronaldo ambaye alikuwa akivaa jezi namba saba.

Alizaliwa mwaka 1984 katika eneo moja la watu masikini wa kabila dogo Kaskazini mwa Uganda.

Hajaoa na anatarajia kufanya hivyo pindi mambo yatakapomwendea vizuri.

Anasema anayafurahia maisha ya kisoka ya Hapa Tanzania tofauti na Uganda kutokana na mashabiki jinsi wanavyoupenda mchezo wa soka na wana ushirikiano na wachezaji.

Kocha Mkuu wa Uganda, Bobby Williamson akimzungumzia Okwi alisema timu yake ilitwaa ubingwa, lakini hajaona bao kali kama alilofunga Okwi katika mechi ya fainali dhidi ya Rwanda.

Mshambuliaji huyo aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Massa Godfrey na dakika ya 74 alipougusa mpira wake wa kwanza aliwaburuza mabeki wawili wa Rwanda kwa kuwapiga chenga akiwa katika kasi na kuachia fataki lililojaa wavuni.

Kitendo hicho kilikuwa cha haraka sana na kiliwafanya mashabiki wa Uganda 'kupandwa wazimu' na kuanza kuimba jina lake huku wakishangilia.

"Alifunga bao zuri sana kwa haraka ambayo sikutarajia, alinisikiliza na kuelewa nimemtuma akafanye nini uwanjani," alisema Bobby, raia wa Scotland.

"Ni mchezaji ambaye alikuwa anaanzia benchi, lakini kila anapoingia anafanya mambo mazuri, katika michezo yote aliyoingia amefanya kazi nzuri sana.

"Hakuingia kwenye kikosi cha kwanza kwavile nilikuwa na mipango mingi na yeye, anaelewa kwanini hakuwa akianza, lakini ni mchezaji mzuri sana ambaye atacheza soka kwa muda mrefu.

"Unajua unapokuwa kwenye kikosi chenye wachezaji wengi na wazoefu kama Uganda inabidi ukubaliane na lolote. Yeye ni mchezaji mdogo bado na anaelewa hali ilivyo."

Kocha huyo alisema kuwa mchezaji huyo amekuwa akifanya mambo makubwa kila anapomuingiza uwanjani kipindi cha pili lakini bado anahitaji kuongeza juhudi kujihakikishia namba kikosi cha kwanza.

Mmoja ya sifa ya Okwi ni kucheza mpira wa kasi na chenga za maudhi jambo ambalo limewafanya mashabiki wa Simba wawe wanamuita "Kwi! Kwi!"

No comments:

Post a Comment