KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, May 21, 2010

Ajisalimisha polisi baada ya kutupa mtoto


JESHI la Polisi Mkoani Pwani, linamshikilia Eliza Mwalongo [20] aliyetupa kichanga mwenye umri wa siku tano mwishoni mwa wiki iliyopita huko Kibaha Kwa Mfipa.

Msichana huyo alitupa kichanga hicho njiani Mei 14 , mwaka huu, majira ya saa 12 asubuhi, na kumfunika kwa majani na miba na kilionekena na wapita njia waliopita katika njia hiyo na kutoa taarifa kituo cha polisi.

Baada ya kupatikana kwa taarifa hiyo kituo cha polisi msichana huyo aliamua kujisalimisha mwenyewe katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kwa Mfipa na baadae kupelekwa kituoni kwa mahojiano zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw. Absaloom Mwakyoma amesema msichana huyo anahojiwa na baadaye atapelekwa kwa daktari ili akapimwe akili zake kama ziko sawasawa na mara baada ya uchunguzi msichana huyo atafikishwa mahakamani.

Msichana huyo alikuwa ni msichana wa kazi za ndani kwa Meja Mstaafu Lekule ambaye alikuwa akimfanyia kazi za mstaafu huyo lakini alikuwa akiishi kwake.

Kamanda alisema msichana huyo alitokea nyumbani kwao Iringa kuja kutafuta maisha ambapo tayari alishakuwa na mtoto mmoja ambaye alitengana na baba yake baada ya ugumu wa maisha ndipo alipokuja huku na kukutana na mwanaume aliyemzalisha na kuishi nae lakini alimkataa baada ya kuzaa mtoto huyo.
.
Kamanda Mwakyoma amesema kuwa, alipoulizwa ni kwa nini aliamua kufanya kitendo hicho alijitetea kuwa alifikia uamuzi huo kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili kwa kuwa alikataliwa na mwanaume aliyemzalisha mtoto huyo.

Pia alisema asingeweza kumuhudumia mtoto huyo kwa kuwa tayari ana mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu na hakuwa na ndugu yoyote wa kumsaidia.

Kichanga hicho cha kiume kilizaliwa Mei 10, mwaka huu, na kimechukuliwa na hospitali ya Tumbi na kinaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment